16 May 2011

Singida, Ilala kufungua robo Kili Taifa Cup

Na Zahoro Mlanzi

TIMU za Mikoa wa Singida na Ilala, zinatarajiwa kufungua robo fainali za mashindano ya Kombe la Taifa (Kili Taifa Cup), itakayoanza kupigwa Mei 22, mwaka huu saa nane mchana Uwanja wa
Kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na kusainiwa na Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema mechi ya pili itakuwa ni saa 10.00 jioni kati ya Mwanza na Arusha.

Alisema siku inayofuata itapigwa robo nyingine kati ya Mbeya na Ruvuma (Ruvuma Warriors) mchezo utakaofuata utakuwa kati ya timu ya Taifa chini ya umri wa miaka 23 (U23) na Kagera (Lweru Eagles).

"Nusu fainali ya kwanza itakayohusisha washindi wa robo fainali za Mei 22 itachezwa Mei 24 na ya pili itachezwa Mei 25 wakati Mei 26 itakuwa mapumziko na mechi ya mshindi wa tatu itakuwa Mei 27 na fainali itachezwa Mei 28," alisema Wambura.

Alisema waamuzi watakaochezesha hatua hiyo ni wale wote wenye beji za Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambao ni Israel Mujuni, Judith Gamba na Oden Mbaga na wasaidizi ni ni Samwel Mpenzu, Hamis Chan’gwalu, Saada Tibabimale, Zahra Hussein, John Kanyenye na Erasmus Jesse.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Mashindano ya TFF iliyokutana jana ilipitia taarifa za michuano hiyo hatua ya makundi ikiwemo malalamiko ya timu za Mara na Dodoma ambazo zililalamikia usajili wa mchezaji mmoja katika timu za Kigoma na Kagera.

Kwa mujibu wa Wambura, alisema kamati haikusikiliza malalamiko hayo kwa vile yaliwasilishwa nje ya muda wa pingamizi.

No comments:

Post a Comment