02 May 2011

Simba safi Kagame Cup

Na Zahoro Mlanzi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limethibisha ushiriki wa timu ya Simba katika michuano ya Kombe la  Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati
(Kagame Cup), itakayofanyika nchini Sudan.

Kombe hilo limepangwa kuanzia kuchezwa Juni 21 mpaka Julai 5, mwaka huu, huku Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), likinogesha mashindano hayo kwa kualika timu mbili kutoka Misri na Ghana.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura, alisema tayari wamethibisha ushiriki wa Simba katika michuano hiyo, ambapo juzi ilikuwa mwisho wa kuthibitisha.

"Jana (juzi), ndio ilikuwa mwisho wa kuthibitisha kwa timu zitakazoshiriki Kagame Cup, na tumefanya hivyo kwa niaba ya Simba, hivyo kilichobaki wafanye maandalizi ili wakaiwakilishe nchi vizuri," alisema Wambura.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hivi karibuni na Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholaus Musonye,  alisema timu za Al Ahly kutoka Misri na Liberty kutoka Ghana, ndizo timu zilizoalikwa katika michuano hiyo.

Awali, mashindano hayo yalipangwa kufanyika visiwani Zanzibar, lakini Chama cha Mpira wa Miguu Zaanzibar (ZFA), kilishindwa kupata wadhamini, ndipo kundi la matajiri la El Mereikh la Sudan, likaamua kubeba jukumu hilo.

Baada ya kundi hilo kuingia mkataba na CECAFA wa kulipa gharama zote zinazohitajika zikiwemo kulipia tiketi za ndege kwa timu shiriki, waamuzi na viongozi wa CECAFA, malazi na huduma nyingine, ndipo walipoamua yafanyikie Sudan.

Bingwa mtetezi wa mashindano hayo ni APR kutoka Rwanda, ambayo ilitwaa ubingwa baada ya kuifunga St. George kutoka Ethiopia mabao 2-0, na mwaka huu inatarajia kutetea ubingwa wake.

No comments:

Post a Comment