02 May 2011

Julio: Tulicheza chini ya kiwango

Na Addolph Bruno

KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya taifa ya vijana 'Vijana Stars', Jamhuri Kihwelu 'Julio', amekiri wachezaji kucheza chini ya kiwango walipoumana na Uganda, juzi
jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Vijana Stars ilikubali kuchapwa mabao 3-1 dhidi ya Uganda 'The Cobs', katika mechi ya marudiano ya kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika 'All African Games',  baada ya awali kufungwa mabao 2-1, wakiwa ugenini.

Akizungumza Dar es Salaam jana, alisema ameshangazwa na kiwango cha chini kilichooneshwa na wachezaji wake katika mchezo huo na hakutegemea hali hiyo kujitokeza.

"Tumefungwa tukiwa nyumbani, lakini ninachoweza kusema, haya ni matokeo ya mchezo ingawa vijana leo (juzi) walicheza katika kiwango ambacho si cha kufurahisha sana na hata mimi nimeshangaa," alisema Julio.

Alisema ameyapokea matokeo hayo kama changamoto kuelekea katika mchezo wa raundi ya pili wa kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Olimpiki dhidi ya Nigeria.

Julio alisema pamoja na kufungwa na kuondolewa katika michuano hiyo kwa jumla ya mabao 5-2, hawatakata tamaa na sasa nguvu zao wanazielekeza katika mechi dhidi ya Nigeria ya kusaka tiketi ya Olimpiki London, Uingereza mwakani.

Alisema anawaomba watazania na wadau wa soka kuendelea kuwaunga mkono katika kipindi cha maandalizi kwani kwa kufanya kinyume, watawaondoa katika hali ya mchezo.

"Tunalazimika kufanya maandalizi ya kutosha kuikabili Nigeria, kwani mchezo huo unaweza kuwa mgumu zaidi ya huu (wa juzi), na hata ule wa Cameroon, tunawaomba wadau wa soka, na TFF, kuendelea kutuamini," alisema kocha huyo.

2 comments:

  1. MPIRA SIO SIASA,MPIRA SIO KITU CHA KUAANZA LEO.
    wachezaji wenyewe umri uliisha pita,umri unaotakiwa.
    WANANCHI tunapenda mpira lakini mpira wenyewe ni wa mwaka 1947.
    TUANZE KUJIPANGA UPYA TUNA MIAKA KUMI.

    MUHIMU KWA SERIKALI NA TFF KUWAAJILI MAKOCHA WAZALENDO KUFUNDISHA MPIRA TIMU YA TAIFA KWA SABABU KOCHA MZUNGU MAZINGIRA YA TZ HAYAJUI yaani wachezaji wetu nategemea kocha kama mzalendo awezi kufungwa na uganda kenya na msumiji kwa kuwa wameisha cheza nao na wanajuana

    ReplyDelete
  2. Sio kweli tutafanya vizuri tukiwa na makocha wazalendo.Tulishakuwa nao miaka mingi sana na nini kilishafanyika kulinganisha na hivi sasa.Mtoa maoni hapo juu unamaana kila siku tutakuwa tunacheza na kenya,Uganda na Msumbiji tu.Vipi kuhusu timu za Afrika magharibi pamoja na Kaskazini ya Afrika?Bado tunahitaji makocha kutoka nje na pia wazalendo tulio nao wanahitajika kwenda Vyuoni zaidi.Tuache mpira wa kuzungumza midomoni.

    ReplyDelete