09 May 2011

Simba kuwapeleka Shiboli, Mkina Coastal

Na Zahoro Mlanzi

KLABU ya Simba, inatarajia kuwatoa kwa mkopo washambuliaji wake Ali Ahmed 'Shiboli' na Shija Mkina kwenda Coastal Union ya Tanga kwa ajili ya kuichezea katika
Ligi ya Kuu ya Tanzania Bara msimu ujao.

Coastal Union ni moja kati ya klabu kongwe nchini ambayo imepanda daraja kucheza Ligi Kuu, hivi sasa ipo katika harakati za kukisuka kikosi chake ili kilete ushindani katika ligi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopatika jijini Dar es Salaam jana na kuthibitishwa na mmoja wa Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo, ambaye hakupenda jina lake litajwe, alisema mazungumzo bado yanaendelea kati ya timu hizo, lakini mambo ya msingi tayari wameshamalizana.

"Ni kweli mpango huo upo kwani tunataka tuisuke upya timu yetu, wapo wachezaji wengi msimu huu tutawatoa kwa mkopo wakiwemo akina Shiboli na Mkina, ambapo hawa wanaweza kwenda Coastal Union ya Tanga," kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kilisema wachezaji hao waliwasaidia kwa kiwango kikubwa msimu uliopita, lakini wanataka wawasaidie zaidi huko mbele na ndiyo maana wameamua kuwapeleka Coastal, ili wakanoe makali yao.

Kilisema Shiboli anatakiwa acheze mara kwa mara, hivyo atakapozidi kukaa nje ya uwanja bila kucheza kiwango chake kitashuka na ana imani wachezaji hao wataisaidia sana timu hiyo.

Mjumbe huyo alimtolea mfano mchezaji Ulimboka Mwakingwe ambaye msimu uliopita aliichezea Majimaji ya Songea, kuwa kiwango chake kimeongezeka na ameisaidia timu hiyo kwa kiasi kikubwa ambapo naye wana mpango wa kumrudisha.

Klabu za ligi Kuu na Daraja la Kwanza hivi sasa zipo katika hekaheka za kusaka wachezaji watakaowasidia kwenye mashindano yao ambapo dirisha la usajili litafunguliwa rasmi Juni 20, mpaka Julai 20, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment