09 May 2011

AC Milan yatangaza ubingwa Italia

ROME, Italia

TIMU ya AC Milan, imemaliza kipindi cha miaka mitano ikiwasindikiza wapinzani wao  Inter Milan, baada ya kutwaa ubingwa wa ligi ya Serie A kwa mara ya kwanza tangu
mwaka 2004 baada ya kutoka suluhu na AS Roma.

AC Milan inayomilikiwa na Waziri Mkuu wa Italia, Silvio Berlusconi ilifanikiwa kutwaa ubingwa huo usiku wa kuamkia jana hivyo kuifikia Inter Milan, ambayo imeshatwaa ubingwa huo mara 18.

“Kutwaa ubingwa baada ya miaka saba ni faraja kubwa,” alisema kiungo wa timu hiyo  Gennaro Gattuso.

Kwa matokeo hayo AC Milan, imefikisha pointi 78 huku ikiwa bado na mechi mbili kibindoni  na haiwezi kupitwa na timu inayoshika nafasi ya pili Inter Milan, ambayo ipo nyuma kwa pointi tisa na jana ilikuwa ikiikaribisha Fiorentina.

Mechi hiyo ambayo ilifanyika kwenye Uwanja wa Stadio Olimpico, ilihudhuriwa na mashabiki 80,000 wakiwemo 10,000 wa AC Milan ambao walikuwa wakishangilia kwa kuwasha fataki zenye kutoa moshi kama wa rangi za bendera ya Italia.

“Wakati huu ni muhimu sana na umekuja baada ya miaka saba,” alisema kingo mwingine wa AC Milan Clarence Seedorf. “Kundi hili litapata mengi baada ya kupata ubingwa huu. Na kwa sasa tunataka kuleta nyumbani ubingwa wa Kombe la Italia,” aliongeza.

Katika mchezo huo timu hiyo nusura ipate bao kipindi cha pili, lakini shuti lililoachiwa na mshambuliaji Robinho likagonga mwamba.

No comments:

Post a Comment