24 May 2011

Shyrose ashupalia adhabu ya Azzan

Na Mwandishi Wetu

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Shyrose Bhanji jana aligeuka mbogo kwenye kikao cha halmashauri hiyo kutokana na
agenda iliyopenyezwa ya baadhi ya wajumbe kutaka mbunge wa Kinondoni, Bw. Iddi Azzan asamehewe adhabu kufuatia kauli yake ya hivi karibuni kudai wajumbe wa sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam ni mafisadi hivyo hawana budi kujiuzulu.

Habari zinasema, wabunge wawili kutoka majimbo mawili ya mkoa wa Dar es Salaam ndio walikuwa mstari wa mbele kumtetea, Bw. Azzan pamoja na Katibu wa Wazee Mkoa, Bw. Mohammed Mtulya.

Hata hivyo baada ya Mwenyekiti wa Wazee kuomba Bw. Azzan aombe radhi ili aweze kusamehewa, ndipo inadaiwa Bi. Shyrose alisimama na kupinga vikali hoja ya mwenyekiti na wajumbe wengine kwa kusema kuwa Bw. Azzan ni vema akathibitisha kauli yake vinginevyo aendelee kutumikia adhabu hiyo.

Kikao hicho kilichofanyika juzi katika Manispaa ya Kinondoni kilikuwa maalumu kutathmini uchaguzi mkuu uliopita mwaka jana. Hata hivyo kikao kilitawaliwa na malumbano kati ya kundi la Bw. Azzan na kundi la Shyrose baada ya kundi la Azzan kudaiwa kutaka asemehewe adhabu hiyo.

"Tuacheni kuwa wanafiki haiingii akilini kwa baadhi ya wajumbe wenye akili zao timamu kusimama na kuanza kumtetea Iddi Azzan...Iddi ametoa tuhuma nzito kwamba Sekretarieti ya Mkoa kuwa ni mafisadi sasa athibitishe kauli yake vinginevyo kwa kiongozi kama yeye kutoa maneno ambayo hayana ukweli ni sifa mbaya," mmoja wa wajumbe alimkakariri Shyrose akilalamika kwenye mkutano huo.

Inadaiwa kwamba Bi Shyrose ambaye alishindwa kwenye kura za maoni jimbo la Kinondoni, alimtaka Katibu wa Wazee Mkoa wa Dar es Salaam kutoyumba katika kuitumikia nafasi hiyo vinginevyo atajishushia heshima kwa kuendekeza masuala ambayo hayana tija kwa chama.

Malumbano kati ya kambi ya Bw. Azzan na Bi Shyrose yaliteka mkutano huo na kujikuta ukiacha ajenda ya msingi ya uchaguzi.

No comments:

Post a Comment