Na Flora Amon
KAIMU Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Said Sadick amesononeshwa na kitendo cha baadhi ya wabunge mkoani humo kutoudhuria Vikao vya Ushauri vya
Mkoa (RCC).
Akizungumza wakati wa ufunguzi ya kikao hicho jana, Bw. Sadiki alisema kuwa inashangaza kuona wabunge ambao ndiyo wahusika wakuu wamekuwa hawaudhurii hata vikao vya bodi ya barabara badala yake watendaji wa serikali ndiyo wamekuwa wakiudhuria.
"Hivi unajuwa hatuwatendei haki waliotupa dhamana hii, wabunge mpo 19 lakini wabunge watano tu ndiyo wameudhuria, angalau mngefika hata nusu, nikiangalia naona mpo watano na tumekaa zaidi ya saa moja na nusu kusubiri wengine.
Baadhi ya wabunge waliohudhuria ni Suzan Lyimo - Viti Maalumu (CHADEMA), Angela Kagaruki-Viti Maalumu (CCM), Halima Mdee-Kawe (CHADEMA), John Mnyika-Ubungo (CHADEMA).
Mkuu wa Mkoa alisema mahudhurio hayo hafifu yanaweza kuathiri maamuzi. "Hata tukiwa tunatoa maamuzi ya pamoja sijui itakuwaje maana tupo wachache, mnapokuwa wachache maamuzi yetu yakapishana mnaweza kusema mimi sijakubaliana wakati hukuhudhuria," aliongeza.
Alibainisha kuwa wabunge na mameya ndiyo wahusika muhimu katika kikao hicho lakini wabunge wamekuwa na maudhurio hafifu hata kwenye kikao cha kamati ya bodi ya barabara.
"Unajua sisi tunaotoka mikoani tuheshimu sana hivi vikao na hata vikianza wakati wa bunge, mbunge akiwa bungeni anaweza kuomba ruhusa kuja kuhudhuria kwani ndiyo vinavyojadili maendeleo na changamoto za mkoa, nyinyi wabunge ni muhimu sana katika vikao hivi," alisema Bw. Sadiki.
Alibainisha kuwa iwe mara ya mwisho kwa wabunge kukwepa vikao vya kamati ya ushauri ya mkoa ili waweze kufanya maamuzi kwa pamoja.
Aidha Bw. Sadiki alizungumzia mfumuko wa bei ambapo alisema kuwa serikali imeruhusu hifadhi ya chakula kufungua milango kwa kuuza mahindi badala kusubiri janga la njaa, hivyo akawataka mameya kuwahamasisha wafanyabiashara wadogo kununua mahindi katika hifadhi ya taifa kwa bei ndogo ya sh. 380 ili wawauzie wananchi.
No comments:
Post a Comment