24 May 2011

Kamati yataka orodha ya wadaiwa sugu TBC

Gladness Mboma na Angelina Mganga

KAMATI ya Bunge ya Mashirika ya Umma imeutaka uongozi wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kuwasilisha majina ya wadaiwa sugu, zikiwamo taasisi za
serikali na binafsi leo saa tano asubuhi.

Mbali na hayo, Ijumaa kamati hiyo itawaita Waziri wa Fedha na Uchumi na Katibu Mkuu wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari na Michezo na Bodi ya TBC kutoa ufafanuzi juu ya madeni hayo sugu.

Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Bw. Deo Filikunjombe aliyasema hayo wakati kamati hiyo ilipokuwa ikipitia nyaraka mbalimbali za mahesabu za shirika hilo, ambapo walibaini uzembe katika ukusanyaji madeni, ambao unatishia shirika hilo kufa.

Bw. Filikunjombe alisema kuwa Ijumaa wiki hii ndio watakutana na viongozi hao kuzungumzia mustakabari mzima wa shirika hilo ambalo 'linaelekea kufa kutokana na madeni mengi'.

Mbunge huyo alikwenda mbali zaidi, akisema kuwa kubadilishwa kutoka Taasisi ya Utangazaji Tanzania (TUT) hadi Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ilisababisha shirika hilo kuyumba kutokana na jina lenyewe lilivyo.

"Kama ningepewa fursa ya kuchagua jina nisingekubali jina hilo kwa sababu siyo la kizalendo, bali ni la Kiingereza na ndio maana shirika hili linayumba katika kazi zake kutokana na jina lenyewe jinsi lilivyo," alisema Bw. Filikunjombe.

Naye Mbunge wa Viti Maalum Ester Bulaya akichambua nyaraka hizo  aliutaka uongozi huo kuwa wazi kueleza kinachowasibu ili kamati hiyo iweze kuwasaidia na kuacha kutoa kauli ambazo hazieleweki.

"Sisi tupo kwa ajili ya kusaidia shirika, wekeni kila kitu wazi, mwanzo mlisema mnadai nje sh. bilioni 5.5 na sasa hivi mnafafanua kwamba mnadai milioni 300, sasa hapo madeni yenu yanakuwa na utata, wekeni mambo wazi ili tuwasaidie," alisema.

Bi. Bulaya aliutaka uongozi huo wa TBC ueleze kamati hiyo wamejipanga vipi katika ukusanyaji wa mapato hayo na kama kuna vikwazo pia waeleze na kuweka wazi, ili kuhakikisha linasonga mbele.

Naye Mbunge wa Mwibara, Bw. Alphaxard Lugola alisema kuwa kamati hiyo haiwezi kukubali fedha nyingi kukaa nje namna hiyo na kwamba kama hali hiyo itaendelea kuwa hivyo shirika hilo litafungwa au kufa.

"Mashaka niliyonayo ni mwenendo wa ukusanyaji wa mapato, ili TBC isianguke lazima mapato yakusanywwe vizuri na inaonyesha wazi kwamba mna hali isiyoeleweka vizuri kutokana na mkataba wa ubia wa matangazo mlionao na Star Media," alisema.

Bw. Lugola alitaka kujua ubia walionao TBC wameainisha vipi, na ni maeneo gani walipaswa kulipa, na kwamba mwanzo ilipoanza ilifanya vizuri na walikuwa na matangazo mengi lakini ghafla hali ilikata na yote hiyo inatokana na ukosefu wa mapato.

Alisema kuwa ukitaka kuona shirika lililo safi unaona ujumla wake na linapofanya mikataba ya ajabu mwisho wake linakufa.

Bw. Kugola alisema nyaraka hizo zinaonyesha kwamba TBC wanadaiwa na Star Media sh. milioni 334, ambapo aliutaka uongozi huo kuipa kamati hiyo mkataba wa Star Media ili waweze kuuangalia na kuwasaidia ili shirika hilo lisifike mahali pabaya zaidi.

Akizungumzia mkataba huo, Mkurugenzi wa Bodi TBC, Bw. Wilfred Nyachia alisema mkataba huo wa ubia unasema kuwa TBC itasaidia Star Media kufanikisha shughuli zake, lakini TBC ilichelewa au kusita kuingia makubaliano nao kwa njia ya maandishi.

Alisema kuwa TBC inadai madeni kwa taasisi za serikali na binafsi na taasisi hizo zimeahidi mwaka ujao wa fedha watawalipa madeni yote, na kwamba kwa saa wametafuta Kampuni ya Majembe Action Mart kwa ajili ya kukusanya madeni hayo.

"Suala la madeni ni tatizo sugu na ni ya kurithi tangu mwaka 2007, madeni ambayo yanafikia sh. 800 na madeni hayo yana matatizo ya nyaraka na wahusika wengi wanaodaiwa hawapo na taasisi zinazodaiwa zilikwishaondolewa, hivyo kusababisha madai hayo kuwa magumu," alisema.

Alisema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana madeni hayo yamepungua kutoka sh. bilioni 5 hadi kufikia sh. bilioni 4.8 na kwamba TBC wana kitengo maalumu cha kukusanya madeni hayo na kwa sasa hawatoi huduma kwa taasisi zinazodaiwa.

No comments:

Post a Comment