Na Anneth Kagenda
WATENDAJI wa Manispaa ya Kinondoni, wameonywa kuwa endapo watabainika kuchukua rushwa kwa ajili ya kufanya udanganyifu kuhusu ardhi ya mtu, sheria
itachukua mkondo wake.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam jana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Goodluck Ole Medeye, wakati wa kufanya majumuisho ya ziara yake ya siku mbili iliyohusu kubaini wavamizi wa maeneo ya wazi na maeneo ya watu.
Alisema kuwa umefika wakati watendaji kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa ili kuwabaini watu hao na pale wanapokuwa wamebainika sheria ichukue mkondo wake haraka ili waweze kuondoka eneo hilo ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja na kuvurugika kwa amani.
"Acheni ubinafsi, huruma na kupokea rushwa, mtu anapobainika kavamia eneo la mtu aondolewe haraka iwezekanavyo na yule atakaye bainika amejenga nyumba kinyume na sheria, basi apewe siku saba awe amevunja na kama hatofanya hivyo, basi tutavunja wenyewe kwani hata kama ni gorofa 10," alisema Bw. Ole Medeye.
Aliwataka viongozi hao kuhakikisha wanawadhibiti wawavamizi wa ardhi na ikiwa hawatafanya hivyo, wanaiongezea serikali mzigo na kusema kuwa hakuna anayeogopa kusikiliza kesi za viwanja mahakamani.
Naibu Waziri huyo aliwatuhumu watendaji hao kuwa hawako makini katika kutunza kumbukumbu jambo linalosababisha kuwepo na usumbufu kwa wananchi pale wanapoleta taarifa zao na badaye hazifanyiwi kazi.
"Kaeni kama timu, wapeni motisha wafanyakazi, tunzeni kumbukumbu za yale mnayoyafanya kwani Manispaa kubwa kama hii halafu inashindwa kutunza kumbukumbu ni jambo la kushangaza, hivyo katika kuhakikisha kunakuwepo na uboreshaji wa kazi, lazima mambo kama haya yazingatiwe," alisema.
Pia aliwataka watendaji hao kutotoa vibali kwa mtu yeyote vya kujenga bila kufanya ukaguzi wa mazingira na kusema kuwa kufanya hivyo ndiko kunakosababisha kuwapo migogoro kama hiyo na wakati mwingine kusababisha vifo.
Alisema atahakikisha haki inatendeka kwa wananchi na wale wamiliki wa viwanja ikiwa ni pamoja na kukomesha rushwa iliyokidhiri kwa baadhi ya watendaji kwa kuishirikisha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Mbunge wa Jimbo la Kawe Bi. Halima Mdee, alisema kuwa umefika wakati kila mtu kuwajibika kwa wakati wake ili kuhakikisha wananchi wanapata maendeleo kama ambavyo waliahidi wakati wa kufanya kampeni huku wakitendewa haki kwenye viwanja vyao na badaye kupata makazi kuliko kuendelea kuhangaika kama hali ilivyo sasa.
"Lazima tuangalie pande zote mbili ili kujua ni kwa jinsi gani tutatatua matatizo sugu ya wananchi kwani hakuna haja ya wananchi kuendelea kulalamika kila siku wakati serikali yao inafanya kazi," alisema Bi. Mdee.
Naibu Waziri alifanikiwa kutembelea baadhi ya maeneo yakiwemo ya Chasimba, Madale, Mivumoni, Bonde la Mpunga, Viwanja vya Tanganyika Packers Kawe, Kilongawima, Kunduchi, Kiwanda cha Saruji, Nyakasangwe na Nakalekwa.
Serikali yenyewe ndiyo yenye kuendeleza ufisadi wa ardhi, sasa inahadharisha nini? Wenye kutapeli na kudalali ardhi za watu ni watumishi wa serikali na vigogo wake, lakini hakuna anayeshikwa na kushtakiwa. Ndiyo bongo hiyo. Usanii mtupu.
ReplyDelete