06 May 2011

Wakunga watakiwa kuafuta maadili

Na Benjamin Masese

SERIKALI imewataka wakunga na wauguzi wa hospitali zote nchini kufuata taratibu na maadili ya kazi zao wakati wa utoaji huduma kwa wagonjwa kutokana na
sekta hiyo kugusa kila mtu.

Vile vile imewaonya baadhi ya wakunga na wauguzi kuacha mara moja vitendo vya kuwatoza fedha mama wajawazito, wazee na watoto wanapohitaji tiba hiyo kwa kuwa wanafanya kinyume na maagizo ya serikali.

Hayo yalisemwa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa kinga kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dkt. Domian Mbando wakati wa kilele cha siku ya wakunga  duniani yaliyoadhimishwa kitaifa Dar es Salaam.

Dkt. Mbando alisema kuwa kumekuwepo na malalamiko mengi juu ya lugha chafu zinazotolewa na wahuduma katika vituo vya afya hapa nchini na kuongeza kwamba serikali itawafukuza kazi iwapo itajihidhirisha na maelezo ya mlalamikaji yatakatolewa.

"Naombeni wakuu wa hospitali na vituo vya afya muwe wakali pia wabainisheni wazi wale wachache wanatumia nafasi zao kuchafua taaluma hii,tunafahamu mazingira mnayofanyia kazi ni magumu na changamoto zake lakini lazima tubadilike na kuachana na kauli mbaya kwa wagonjwa,"alisema.

Dkt. Mbando alisema moja ya mikakati ya serikali iliyopo ya kuhakikisha huduma inakuwa karibu na wananchi ni pamoja na kuongeza vitendea kazi, kuboresha mazingira, kuongeza shule na vyuo na wataalamu wa mafunzo.

Hata hivyo alisema kuwa kutokana na takwimu zilizopo zinaonesha kwamba idadi ya vifo vya akinamamam wajawazito vimepungua kutoka 578 mwaka 2005 hadi 454 mwaka 2010 kati wajawazito 100,000.

Dkt. Mbando alisema kuwa mbali ya vifo hivyo kupungua lakini bado tatizo hilo ni kubwa kutokana na tafiti kuonesha kwamba asilimia 98 za mama wajawazito hufika hospitali kuangalia afya zao ambapo wanaojifungulia hospitalini ni asilimia 40 na kati ya hao asiliamia 15 hupata matatizo ya uzazi yanayotishia maisha.

Alisema tatizo la akimama kutojifungulia hospitali linachangiwa na wanaume kutoshiriki na kuhamasisha katika suala zima la afya ya uzazi.

Naye Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania (TAMA), Bi. Feddy Mwanga alisema changamoto zinazowakabili ni uhaba wa watoa huduma hususan wakunga, mazingira ya kufanyia kazi sehemu nyingi kuwa duni na upungufu wa vitendea kazi kitendo kinachoathiri kiwango cha huduma zinazotolewa.

Vile vile alisema wakunga wamekuwa katika kundi lisilodhaminiwa  katika jamii huku likiwa katika lawama nyingi kuliko kutambua kazi nzuri inayofanywa na kundi hilo tena katika mazingira magumu.

No comments:

Post a Comment