16 May 2011

Sangoma auawa kwa kukataa kupiga ramli

Na Juddy Ngonyani, Sumbawanga

JESHI la Polisi Wilayani Sumbawanga mkoani Rukwa linawashikilia ndugu wawili kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mganga wa kienyeji Amos Kapufi (30) baada ya
kugoma kuwapigia ramli kumpata mwizi wa kuibiwa mpunga wao.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Bw. Isunto Mantage ilisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 11 jioni mara baada ya watuhumiwa hao ambao, Silvanus Mwanandenje (32) na mdogo wake Justine Mwanandenje (28) kwenda kwa mganga huyo na kumtaka awapigie ramli ili waweze kuwabaini watu waliowaibia mpunga wao shambani kwao.

Kwa mujibu wa Kamanda Mantage mganga huyo mkazi wa Kijiji Kaozye, tarafa ya Kipeta wilayani alikataa kutelekeza maombi yao ndipo ukazuka ugomvi wa ghafla na kuanza kumshambulia kwa kumpiga na jiwe kichwani hali iliyosababaisha mauti yake.

Kamanda Mantage amesema kuwa vijana hao bado wanahojiwa na polisi na watapoandishwa kizimbani mara baada ya upelelezi wa jeshi hilo kukamilika.

Wakati huo huo jeshi la  polisi linamshikilia Emmanuel Sadala (32) ambaye ni mganga wa kienyeji pamoja na Frank Malema (31) wote wakiwa ni wakazi wa Kijiji cha Zimba, Tarafa ya Mtowisa wilayani Sumbawanga kwa tuhuma za mauaji ya Thoabias Malama (41) kwa tuhuma za ushirikina.

Kamanda Mantage alisema kuwa marehemu huyo aliuawa Mei 12, mwaka huu majira ya saa 6.30 usiku na watu wasiojulikana baada ya kumvamia akiwa amelala nyumbani kwake na kumshambulia kwa vitu vyenye ncha kali jambo lilolosababaisha kuvuja damu kwa wingi na kufariki dunia.

Hata hivyo, kamanda Mantage alisema kuwa uchunguzi wa awali wa jeshi hilo umebaini kuwa [ tangu Novemba, mwaka jana kulikuwa na mgogor  kati ya marehemu na mdogowe aitwaye Frank Malema aliyeugua kwa muda mrefu na ikadaiwa kuwa alikwenda kwa mganga Sadala kupiga ramli na kuelezwa kuwa amelogwa na kaka yake.

No comments:

Post a Comment