16 May 2011

JK akiri wizara zinanuka rushwa

*Awaagiza watendaji waiokomeshe ili CCM ishinde 2015
*Asisitiza nidhamu ya matumizi ya fedha za walipakodi
*Makamu wa Rais: Ufisadi ulipunguza ushindi wa CCM


Na Pendo Mtibuche, Dodoma

RAIS Jakaya Kikwete amekiri kuwa vitendo vya rushwa vimekithiri katika wizara na idara za serikali na
hivyo kuwaagiza mawaziri, manaibu wao na watendaji wengine wakuu kuisafisha ili Chama Chama Mapinduzi kipewe ridhaa ya kuendelea kuongoza mwaka 2015.

Alibainisha kuwa vitendo vya rushwa hivi sasa vinatendeka ndani ya wizara na idara mbalimbali za serikali hivyo hatua za haraka za kukabiliana na tatizo hilo ni mawaziri, manaibu wao, makatibu wakuu na manaibu wao kujisafisha ili waweze kufanana na mabango yaliyopo katika ofisi zao.

Alisema kuwa ili serikali iliyopo madarakani iweze kuendelea baada ya uchaguzi wake wa 2015 ni lazima viongozi hao waanze kuweka maandalizi mazuri ya uchaguzi unaokuja kwa kujisafisha na rushwa na kujali maslahi ya wananchi wanaowaongoza.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati akifunga semina elekezi kwa viongozi na watendaji wakuu wa serikali ambayo ilifanyika kwa muda wa siku saba mjini Dodoma ambapo rais alisema kuwa semina hiyo imekuwa na mafanikio makubwa ukilinganisha na iliyofanyika Ngurudoto Mkoani Arusha katika kipindi chake cha kwanza.

Rais alisema kuwa katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa viongozi hao wa serikali lazima waweke mbele nidhamu ya matumizi ya fedha za umma, hivyo suala la viongozi kutosimamia vita dhidi ya rushwa kikamilifu katika idara zao ni tatizo.

Alisema kuwa rushwa inayotendekea hivi sasa inatendeka chini ya wizara na idara za chini ambazo viongozi hao wanazifanyia kazi, hivyo lazima viongozi hao wachukue hatua katika kukabilia na vita dhidi ya rushwa.

“Hakuna mtu mwingine anayeweza kupigana na tatizo hilo. Wakati natembelea wizara mbalimbali nilikuwa nakutana na mabango makubwa mbele ya wizara nyingi ambayo yana ujumbe wa unaosema hapa si mahala pa rushwa, ninachowaomba mabango hayo yafanane na mwenendo na tabia halisi ya maneno yaliyopo katika mabango hayo,” alisema.

Alisema kuwa mabango hayo ya rushwa yafanane na tabia na muundo wa wizara husika na afisa anayefanya kazi katika ofisi hiyo lazima aendane na upigaji vita rushwa kwani hakutakuwa na maana kama mabango hayo yataendelea kuwepo kwenye wizara lakini utekelezaji ukawa haupo, hicho kitakuwa ni kiini macho na kichekesho kwa wananchi.

“Piganeni muonekane mnapigana na tatizo hilo na mkifanya hivyo mtakuwa mmefanya kazi kubwa ya kuondoakana na kero hii ya rushwa katika nchi, hivyo lazima mfanye kazi kwa kufuata katiba, utawala wa sheria na taratibu zilizowekwa,” alisema.

Alisema kuwa kila waziri, naibu waziri, katibu mkuu na naibu katibu mkuu anapotoka katika mkutano huo ahakikishe kuwa anaenda kutekeleza suala hilo kwa umakini mkubwa kwani kuondoa rushwa ndani ya maofisi kutawezesha kuwepo kwa utendaji unaojali maslahi ya wananchi.

Alisema kuwa lazima nidhamu ya fedha za umma iwepo kwani wananchi wanapenda kuona ukusanyaji wa mapato unaimarika na kuongeza uwezo wa serikali katika kuongeza mapato ya wananchi.

Rais alisema kuwa wananchi wanatarajia baada ya semina hiyo kumalizika wataona mabadiliko ndani ya serikali kwa viongozi kufanya kazi karibu na nao na kutatua kero zao ili kuwaletea maendeleo.

Alisema kuwa ni lazima viongozi hao wafanye kazi kwa umakini mkubwa wawe wabunifu na wenye kuona mbali zaidi juu ya changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi ikiwa ni pamoja na kuwataka viongozi hao kupanga mipango yao kwa umakini katika sekta za uzalishaji na uchumi katika serikali.

Alirudia kuwakumbusha viongozi hao kutoka katika maofisi yao na kwenda  vijijini kwa wananchi waliko ili kuwasikiliza kero zao na kuwatatulia kuliko kuendekeza kukaa maofisini huku wananchi wakilalamikia huduma.

Alisema viongozi hao ndiyo wenye majibu ya wananchi, hivyo viongozi hao wanapaswa kwenda mikoani wilayani na hata vijijini kwa ajili ya kujionea wao wenyewe kero za wananchi na kuzipatia majibu na kuyatolea taarifa.

Alisema kuwa lazima viongozi hao wajenge tabia ya kutoa taarifa kwenye vyombo vya habari juu ya mambo mbalimbali wanayoyatekeleza na wasiwaache waandishi watafute habari wao wenyewe wakati wao wapo na mamlaka ya kutoa habari wanayo.

Alisema kuwa ili Chama cha Mapinduzi kiweze kushinda uchaguzi 2015 ni  lazima viongozi hao wawajibike kikamilifu kwa kutoa taarifa sahihi za mambo mbalimbali ynayotekelezwa na serikali na hayo ndiyo yatakayokuwa maandalizi mazuri kwa chama hicho katika uchaguzi ujao.

Wakati huo huo, Mwajuma Juma anaripoti kuwa Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi amesema kuwa CCM ilipata ushindi mdogo katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana, kutokana na kushamiri kwa
vitendo vitendo vya ufisadi, vilivyofanywa na baadhi ya viongozi katika kura za maoni.

Balozi Seif alitoa kauli hiyo Kisiwani Pemba wakati akizungumza na viongozi wa chama hicho kufuatia ziara yake ya siku mbili kisiwani humo.

Alisema kuwa katika kura ya maoni ya kuchagua viongozi watakaogombania nyadhifa katika majimbo kulifanyika vitendo vya ufisadi na rushwa na kupelekea wanachama wao wengi kupoteza imani kwa wagombea hao ambao walipita bila ya kuwa na ridhaa zao.

“Tabia ya baadhi ya viongozi kujishirikisha na vitendo vya ufisadi kwa mali za umma kumesababisha wananchi kupoteza imani na chama ndio maana CCM imeamua kujivua gamba kwa kuwatimuwa viongozi wasiokuwa waadilifu,” alisema Balozi Seif.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo chama hicho sasa kimeamua kujipanga upya katika safu zake za uongozi upya, kwa kuzingatia kaulimbiu ya kujivua gamba.

“Lengo kubwa ni kudhibiti njia zote zinazopelekea ushawishi wa rushwa, hasa wakati wa kutafuta viongozi ili waweze kupatikana viongozi waadilifu na wenye kuzingatia misingi ya utawala bora,” alisema Balozi Seif na kuwataka viongozi kuwa makini wakati wa uchaguzi kwa kuwachagua viongozi bora na si bora kiongozi.

Aidha Balozi Seif ambae pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa alisema kuwa CCM haitomvumilia kiongozi yeyote ambaye atabainika ushindi wake umepatikana kwa ushawishi wa rushwa, kwa vile vitendo hivyo vinakwenda kinyume na maadili ya katiba ya chama hicho.

Katika uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka jana CCM ilipoteza viti vitatu katika ngome yake kisiwani Unguja likiwemo jimbo la Magogoni, Mtoni na Nungwi.

9 comments:

  1. Naona mweshimiwa sana naye analalamika sasa sijui mwananchi wa kawaida afanyeje.
    Nikama nchi imebakiwa na Rais jina na siyo Rais mtendaji. Jamani Uraisi siyo kuvaa suti, kuitwa muheshimiwa, kupigiwa saruti,kuweka sahihi kwenye nyaraka za serikali.
    Pole sana Tanzania kazi unayo!

    ReplyDelete
  2. Tuwe na akili na mawazo yaliyokomaa,sio akili uchwara na akili za kuazimwa, hivi Raisi angeweza kufanya kazi pekee mawaziri aliowachaguwa wa nini? ndio maana kila mtu kampa jukumu lake na yeye pekee asingeweza acha utoto huo na chuki binafsi uchizi si kub=vua nguo

    ReplyDelete
  3. Sasa yeye anakiri badala ya kusema amechukua hatua gani!!!???, Tume iliyomuondoa Lowasa madarakani na ikapendekeza ashitakiwe, yeye mwenyewe akasema Lowasa mtu safi kwenye uchaguzi!!!???, huoni kama haya ni maneno tu ya kujikosha, mbona hakuna anayechukuliwa hatua.

    angalieni dhamira ya mtu kabla ya kumuamini.

    ReplyDelete
  4. Hapa tumsaidie Rais wetu si kebeza mambo muhimu kama haya
    Ya watendani ulaji na wazembe.Rais kuna wasomi vijana na wahitimu
    Ndani na nje ya nchi kama wakiendelea kukutegea wewe ndio ufanye
    Kila kitu ni muda sasa wa kuwawajibisha kabla mambo hayajawa
    Mabaya.

    Nimeshuhudia mawizarani/idarani watendani wazuri wanawekwa
    Bench kwa misimamo yake ya kufuata taratibu.hata teuzi mbali mbali
    Zinafanywa kishikaji.Nakupongeza Rais kwa hili.

    ReplyDelete
  5. Mtu yeyote anaye mtetea kikwete utamuona ataanza kutoa comments kwa matusi. Mchangia namba mbili pole tunajua wewe pia mnufaika wa utendaji mbovu wa Kikwete, endelea kuwaita wenzako wajinga kwa vile huelewi kipimo cha ujinga ni pamoja na kuandika lugha ya matusi, mimi nakuona wewe ndo mjinga,

    Sidhani kama inahitaji elimu ya PHD kujua kuwa Kikwete ameshindwa kabisa kuiendelza/kuiongoza Tanzania. Mkapa pamoja na ufisadi lakini aliacha nchi pazuri. ila huyu ndugu yetu uwezo wako ni mdogo sana, ndo maana badala ya kufanya kazi yeye analalamika tu.

    Katika maisha kunabahati mbaya kumpa nchi Kikwete ni bahati mbaya, tulikosea, hatuna la kufanya, kwani ulewa wetu mdogo, umoja hakuna, hivyo tusubili muda wake uishe. Tukiendelea na ujinga huhu hata 2015 tutachagua mtu mwenye uwezo mdogo tena.
    Kazi kwenu

    ReplyDelete
  6. Jamani huyu Mkuu wetu wa nchi naye saa nyingine anashangaza. Uozo ulioko serikalini kumbe anaujua sasa kwa nini hachukui hatua? Yeye ndiye aliyewaweka hawa wanuka rushwa sasa anangoja nini? Chukua hatua au kubali kuwa umeshashindwa kutawala. Hii inatukera sana wananchi wako. Au ni kwa sababu Mkuu wetu tukilia hali ngumu ya maisha yeye haijui hali ngumu? Unatupa hasira saaana sijui tukuambieje Mkuu. KUBALI KUWA UMESHASHINDWA KUTAWALA TZ BWAGA MANYANGA BASI!

    ReplyDelete
  7. CCM is on the defensive,CDM wamewavuruga sasa nao wanavurugana,mimi naamini tatizo la nchi hii si Lowassa hata kidogo,infact watu wengi wanamwogopa akiwemo JK mwenyewe,tunaopenda kufikiri tunaelewa kuwa hata ishu ya Richmond JK alihusika kuipika ili Lowassa atoke kwenye u-PM,lakini dhahabu haina budi kupita kwenye tanuru ili iwe safi...if they knew Jesus was God,they wouln't slap him!!!

    ReplyDelete
  8. Yeye rais si ndio amechangua mawaziri, makatibu wakuu, manaibu waziri sasa anamlalamikia nani? Hicho ni kiini macho kuwaonyesha wananchi kama anapinga rushwa. Kwanza anachojali ni uchaguzi 2015, wala sio maslahi ya wananchi sasa hivi.

    ReplyDelete
  9. Tatizo lako baada ya kupata Urais ukaendeleza tabia ya kisiasa kuwajaza wana siasa katika serikali badala ya kuweka Watendaji,unategemea nn?

    Na unapotulalamikia wananchi tukusaidieje ?Hivi mtoto wako kakushinda unakwenda kumshitakia kwa jirani unadhani atakusaidia nini?
    Je wewe umeshindwa kumkanya mwanao?Kweli wewe ni msanii tu hujui wajibu wako.wewe hufai wala huyo Dr,Slaa hafai nyinyi wote ni wapiga kelele lakini sio watendaji hata kidogo

    ReplyDelete