Na Mwandishi Wetu
MAHAKAMA ya Mwanzo Mingoyo imemuhukumu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkwaya, Bw. John Itumbili kulipa faini ya sh. 1.5 milioni baada ya kupatikana na hatia ya
kuvuruga ndoa ya watumishi wenzake.
Hukumu ilitolewa mwishoni mwa wiki iliyopita na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Bi. Sharifa Mchilowa, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka.
Watumishi hao ni pamoja na mwalimu mwenzake aitwae Zaidatu Said wa Shule ya msingi Mkwaya na Khamisi Mikidadi, Ofisa Afya wa Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.
Kabla ya kutolewa kwa hukumu hiyo, Hakimu Mchilowa alimpa mshtakiwa nafasi ya kujitetea kutokana na kosa linalomkabiri,ambapo aliomba asipewe adhabu kali kwa vile ni kosa la kwanza, ana familia ya watoto wanne na wazazi wanaomtegemea, hivyo kama atapewa adhabu kali kuna hatari wa kukosa mtu wa kuwahudumia.
Hakimu Mchilowa alisema ameusikiliza utetezi wa mshtakiwa, lakini kutokana na kosa alilolifanya kuwa ni kubwa, amelazimika kutoa adhabu kali kwa kumlipa mlalamikaji Khamisi Mikidadi, sh. milioni 1.5 kwa kosa la kumvurugia ndoa yake.
Bw. Mikidadi kwa hivi sasa anahudumu katika Kituo cha Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara na mkewe anaendelea kufundisha katika Shule ya Msingi Mkwaya, iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Lindi.
Awali ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Bw. Itumbili ambaye ni kiongozi katika shule hiyo, amekuwa na mahusiano wa kimapenzi na Zaidatu Said, kwa zaidi ya mwaka sasa, baada ya mume wake, Mikidadi kuwa nje ya kituo chake cha kazi kwa ajili ya masomo, hali iliyochangia kutokuwa na maelewano mazuri na ndoa yake.
Licha ya kuvuruga ndoa hiyo pia, mahusiano hayo yalidaiwa kusababisha pia kuvunjika kwa ndoa ya mshtakiwa huyo, baada ya mke wake Moza Songoni, aliyekuwa akifundisha katika shule hiyo kudai taraka, baada ya kubaini mume wake amekuwa na mahusiano wa kimapenzi na Zaidatu Said.
Mwalimu Moza Songoni, kwa sasa amehamishiwa Shule ya Msingi Mihogoni, iliyopo kata na Jimbo la Mtama.
No comments:
Post a Comment