Na Said Hauni, Kilwa Masoko
HALMASHAURI ya Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, kwa mara nyingine tena imeingia kwenye kashifa ya ufisadi baada ya kutoweka kwa njia ya utatanishi vitabu 101 vya kukusanyia
mapato, na hivyo kuisababishia hasara ya mamilioni ya fedha kipindi cha miaka miwili iliyopita.
Licha ya upotevu wa vitabu hivyo, pia zipo zaidi ya sh. 995,434,069 za ukaguzi wa mapato kwenye Akaunti za Mfuko mkuu, memoranda ya fedha ya Mamlaka za Serikali za mitaa pamoja na mali za kudumu hazijulikani zilipo, kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali za Mitaa mwaka 2009/2010.
Pia ukaguzi wa Stakabadhi za mapato na taarifa za benki za Akaunti ya Mfuko mkuu imeonyesha kiasi cha sh. 149,033,336.0 hazikupelekwa benki, wakati hati za malipo zenye thamani ya sh. 144,994,981 hazikupatikana wakati wa kazi ya ukaguzi huo ukifanyika, na kufanya uhalali wa malipo yaliyofanyika kutothibitishwa.
Taarifa hiyo inaonyesha halmashauri ya Kilwa haikuandaa taarifa ya matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo na ugharimiaji kwa mwaka unaoishia Juni 30/2010, hivyo kukosekana kwa taarifa hiyo, fedha zilizopokelewa na kutumika kwa miradi ya maendeleo hazikuthibitishwa.
Taarifa hiyo imeendelea kueleza kwamba malipo ya jumla ya sh 449,681,752, hayakuwa na viambatanisho, hali inayofanya halmashauri hiyo kukiuka agizo Na.5(c) la memoranda ya fedha ya mamlaka za Serikali za Mitaa mwaka 1997.
Hali hiyo kumeifanya Halmashauri ya Kilwa mkoani Lindi kupata Hati Chafu msimu huu.
Akichangia hoja katika mkutano wa Jumuia tawala za mikoa (ALAT) tawi la Lindi, uliofanyika hivi karibuni mji mdogo wa Masoko, Wilaya ya Kilwa, Ofisa Serikali za Mitaa mkoa wa Lindi, Yohana Paul Miwa, alionyesha kushangazwa na tabia ya upotevu wa vitabu vya kukusanyia mapato, ikiendelea kufanyika katika halmashauri hiyo.
Miwa alisema kutokana na kutoweka kwa vitabu hivyo 101 vya kukusanyia mapato, halmashauri hiyo imekuwa ikipoteza mamilioni ya fedha kila baada ya muda bila ya sababu zozote za msingi.
No comments:
Post a Comment