23 May 2011

Kinyerezi wapinga mradi wa upimaji viwanja

Na Gladness Mboma

WAKAZI wa Kijiji cha Kifuru Kata ya Kinyerezi, Dar es Salaam wamepinga mradi wa viwanja 30,000 ulioanza kufanyika katika kijiji hicho kwa madai kuwa
umeendeshwa kinyume na sheria na una harufu ya ufisadi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano ulioitishwa na Diwani wa Kata hiyo, Bi. Leah Mhutu pamoja na Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa, Bw. Michael Msome wananchi hao walisema kuwa mradi huo una harufu ya ufisadi na unaletwa kwa ajili ya kuwanyanyasa wananchi.

Bw. Mohamed Ally alisema kuwa mpango mzima wa uhakiki wa viwanja, serikali imevunja sheria, kwani walipomaliza uthamini walitakiwa kuwalipa fidia wananchi lakini wamekaa kwa zaidi ya miaka miwili ndipo wanawaletea fomu kuwataka wajaze na kwenda kuzilipia katika Benki ya Wananchi Dar es Salaam kwa sh. 20,000 ili waweze kuuziwa viwanja hivyo.

"Sisi hatukubaliani na hilo, huu mpango ni batili inakuwaje sisi wakazi wa miaka kibao leo hii tuanze kuletewa fomu kujaza na kuuziwa tena nyumba na viwanja vyetu, inashangaza na ninasema nipo tayari kufa kwa kupigania haki yangu," alisema, Bw. Ally.

Naye Bw. Mbonea Silvano alisema ni lazima serikali itambue kuwa watu wa Kinyerezi wana haki sawa zaidi ya 'vyura wa Kihansi' na kusisitiza kwamba huo mradi hawautambui.

"Serikali ni lazima itambue kwamba sisi wananchi hatutaki mauaji yatokee hapa kama yale ya Madale hatutaki kumwaga damu, lakini kama itaendelea kutokuwa sikivu na kusikia kilio chao wasishangae ya Madale yakatokea Kinyerezi," alisema.

Naye Bw. Godlizen Mmary alisema wakati maofisa wa Manispaa ya Ilala walipokwenda kuthamini hawakuwaeleza kama kuna utaratibu wa kuuziwa viwanja kwa mita za mraba mmoja kwa sh. 5,000 na kudai kushangazwa na tangazo lao.

Wakizungumza kwenye mkutano huo, Diwani wa Kata ya Kinyerezi (CCM), Bi. Leah Mhutu, ambaye alipata wakati mgumu wakati akizungumza kutokana na wananchi kumweleza kwamba na yeye anatumika katika mpango mzima wa kuwanyang'anya viwanja vyao, alisema yeye yupo bega kwa bega na wananchi, ambapo aliwaomba ushirikiano.

"Ndugu zangu ninyi ndiyo mlionichagua, siwezi kwenda kinyume na ninyi na ndiyo maana huu mkutano tuliamua kuitisha mimi na Mwenyekiti wenu wa Serikali za Mitaa, ambapo tulimwalika Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala na Ofisa Ardhi, ili watueleze kuhusiana na mradi huu lakini hawakufika.

"Nipeni ushirikiano sitokubali mwananchi wa Kinyerezi, achakachuliwe eneo lake, msijaze fomu mpaka kieleweke, hawa viongozi watakimbia, lakini ipo siku wataingia kwenye 18 zetu watapeleka wapi fomu," alisema.

Alisema kukimbia tatizo si kutatua tatizo, wanachotakiwa ni kwenda kuzungumza na wananchi na kusisitiza kwamba kesi hiyo haiwezi kuishia kwenye makaratasi na kukaa ofisini, bali wanatakiwa kwenda kwa wananchi.

"Ninachoomba msinihukumu mimi na Bw. Msome, bali tujadili nini tufanye kuhusu hawa viongozi ambao tumewapelekea mwaliko, lakini wameshindwa kufika katika huu mkutano muhimu," alisema.

Alisema kinachotakiwa ni viongozi hao kurudi kuzungumza na wananchi na si kukimbia tatizo na kusisitiza kwamba kesi ya shamba inatakiwa kuishia shamba na si vinginevyo.

Naye Bw. Msome ambaye alitakiwa asizungumze chochote hadi atakapoyatoa mazungumzo yake kwa maandishi, aliwaambia wananchi hao kwamba athari hizo hata yeye zinamhusu na ana uchungu kuliko wao wanavyofikiria.

Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, ilitoa tangazo kwa umma kuhusu uuzwaji viwanja katika eneo hilo ikiwa ni mwendelezo wa mradi wa upimaji wa viwanja 20,000 Dar es Salaam.

Katika tangazo hilo walidai kwamba fomu za maombi ya kununua kiwanja zitaanza kutolewa Mei 19 mpaka 25, mwaka huu na mwombaji atatakiwa kulipia ada ya maombi kiasi cha sh. 20,000 katika Benki ya Wananchi Dar es Salaam, fedha ambazo hazitarejeshwa.

Kwa mujibu wa tangazo hilo mtu atatakiwa kulipa sh. 10,000 kwa kila mita moja ya mraba kwa makazi; sh. 15,000 kwa ukubwa huo kwa biashara, na sh. 20,000 kwa huduma za jamii, ibada sh. 8,000 na wenye nyumba waliotambuliwa kabla ya upimaji watatoa sh. 5,000 kwa mita ya mraba.

No comments:

Post a Comment