02 May 2011

Maelfu ya abiria wakwama Ubungo *Ni mgomo wa madereva mabasi ya mikoani

Na Edmund Mihale

ABIRIA waliokuwa wakisafiri kwenda katika mikoa mbalimbali nchini jana  walijikuta katika wakati mgumu baada ya madereva wa mabasi kugoma kwa lengo la kuwashinikiza
waajiri wao kuwapa mikataba ya ajira na maslahi bora kazini.

Mgomo huo uliochukuwa saa saba ulisababisha msongamano mkubwa wa mabasi na abiria katika Kituo Kikuu cha Basi cha Ubungo (UBT).

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana madereva hao walisema kuwa wameamua kugoma wakati wa Sikukuu ya Mei Mosi ili kufikisha ujumbe wao kwa serikali.

Moja wa madereva hao ambaye hakuta jina lake litajwe gazetini alisema kuwa kwa kipindi kirefu wamekuwa wakidai mikataba hiyo lakini wamiliki wa magari hayo wamekuwa wakidharau kuitoa.

"Mfano mimi nimefanya kazi kwa muda wa miaka minne sasa lakini ajira siijui nalipwa kwa trip natoka hapa kwenda Moshi sh. 10,000 nikirudi pia sh 10,000 baada ya hapo hatuajuani na tajiri hadi niendeshe gari tena," alisema.

Alisema wamemua kutumia Sikukuu ya Mei Mosi ili kufikisha ujumbe kwa serikali kwa kuwa wajiri hao wamekuwa wakitangaza kuwa wamewaajiri kumbe si kweli.

Wakati madereva hao wakijinadi kufikisha ujumbe huo kwa serikali kwa njia ya mgomo abiria katika kituo hicho walirusha lawama kwa madereva hao kuwa kwa kufanya hivyo si uungwana kwani hayo ni mambo waliyotakiwa kufanya kabla hawaanza kazi hiyo.

"Hivi madereva hao wameona njia hii ya kutesa abiria ndiyo itakayowatatulia matatizo kati yao na waajiri wao....si halali kutumia mgongo wa mtu mwingine kushinikiza madai yao, haya ya madereva na waajiri wao kwa kweli hayatuhusu," alisema Ismail Ally aliyekuwa akisafiri kwenda Arusha.

Abiria mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Bw. Rutta alisema kilichosababisha mateso hayo kwa abiria ni ulimbukeni wa madereva kutumikia kazi zao hizo kwa miaka bila mikataba na mbaya zaidi wengi wao shule hakuna, hivyo wanastahili kuwezeshwa kielimu ili wajitambue na wabuni njia sahihi za kudai stahili zao na si kama hii ya kutesa abiria.

Dereva mwingine ambaye pia hakutaka kuweka jina lake wazi alidai taarifa ya mgomo huo waajiri wao wanayo siku kadhaa zilizopita bali hawakuamini iwapo kweli watatekeleza azma yao hiyo.

Mgomo huo ulimalizwa na Waziri wa Uchukuzi, Bw. Omri Nundu baada ya kutoa ahadi ya kushughulikia madai yao kwa kipindi cha wiki mbili zijazo.

No comments:

Post a Comment