02 May 2011

Kujivua gamba CCM si kufukuzana-Mahanga

Na Grace Michael

MJUMBE wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa (NEC), Dkt. Makongoro Mahanga ameibuka na kusema kuwa dhana halisi na yenye tija ya
kujivua gamba ni kwa wana CCM wote kujiuliza, kujirudi, kujirekebisha na kuwa na mtazamo chanya wa kukijenga chama.

Alisema kuwa hatua ya kujivua gamba iliyofanywa na chama hicho haikuwa na maana ya kufukuzana kwenye chama au kujiuzulu kwa viongozi au wanachama wachache kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu wakiwemo wana-CCM bali ni hatua za uwajibikaji na maandalizi ya kufikia dhana inayokusudiwa na chama.

Dkt. Mahanga aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na wajumbe wa mashina ya CCM katika Tawi la Ugombolwa, Kata ya Segerea, Dar es Salaam.

"Ili dhana hii ikamilike ni lazima kila mmoja wetu ajirudi na ajiulize ni namna gani alikiumiza chama na baada ya kujiuliza abadilike sasa na kuanza kukijenga chama kwa nguvu zote...kila mmoja akitafakari anaelewa namna alivyofanya, tuangalie sababu zote za CCM kutofanya vizuri kwenye uchaguzi wa mwaka jana na dhana hii si kutazama sababu moja tu na kuishikia bango, lazima tuangalie na kushughulikia sababu zote," alisema Dkt. Mahanga.

Alitumia mwanya huo kuchambua sababu nane kwa wajumbe hao ambazo
zilisababisha CCM kutofanya vizuri katika uchaguzi ambazo ni pamoja na kukua kwa demokrasia ya vyama vingi duniani na Tanzania, makundi na chuki za kisiasa miongoni mwa wana CCM, hali ngumu ya maisha, kupanda bei na ukosefu wa ajira, mfumo mpya wa kura za maoni, kero ya rushwa na ufisadi, rushwa wakati wa uchaguzi na hasa chaguzi za ndani ya chama, rushwa kwenye huduma za wananchi na rushwa ya mikataba ya serikali.

Sababu zingine alizotaja ni kutowatumikia wananchi vizuri na kutotekeleza ilani ya uchaguzi ya CCM, kutowajali wanachama wa chini na viongozi wa mashina pamoja na uchumi dhaifu wa chama hasa ngazi za kata na matawi.

Akizungumzia sababu ya kukua kwa demokrasia, Dkt. Mahanga alisema kuwa
changamoto hiyo inahitaji umakini kwa CCM na kuwa na umoja na mshikamano lakini chama na serikali kuhakikisha inashughulikia kero za wananchi kwa umakini kwa kuwa hali hiyo inachochewa na mtazamo wa kipropaganda duniani wa kutaka kuona vyama vilivyoshiriki katika kupigania uhuru wa nchi za Afrika vinaondolewa madarakani.

Kuhusu makundi na chuki za kisiasa miongoni mwa wana-CCM, aliweka wazi kuwa
chama kinakabiliwa na ugonjwa mbaya kama kansa wa kujenga makundi yenye chuki ya kudumu wakati wa uchaguzi hasa wa ndani kwa kuwa kumekuwa na mwendelezo wa makundi hata baada ya washindi au wateuliwa ndani ya chama kupatikana.

"Tunapoingia kwenye uchaguzi wa dola bado baadhi ya viongozi na wanachama
hawavunji makundi na wengine hawashiriki kabisa kwenye kampeni za chama na
wengine wanadiriki kuhujumu ushindi wa CCM kwa kuwapinga wana-CCM wenzao hata kuwapigia kura wapinzani kutokana na makundi, chuki zinazotokana na kura za maoni hili ni tatizo ambalo limekiumiza sana chama na NEC imelikemea vikali na kuonya chini ya Mwenyekiti wetu Rais Jakaya Kikwete," alisema Dkt. Mahanga.

Akielezea sababu ya hali ngumu na kukosekana kwa ajira, alisema kuwa ukosefu wa ajira hasa kwa vijana na mishahara isiyokidhi mahitaji imezidisha ugumu wa maisha na katika hali hiyo ya kukata tamaa, wananchi na hasa vijana wamekosa imani na serikali na chama kilicho madarakani hivyo kukiathiri chama katika uchaguzi.

"Pamoja na tatizo hili kuwa ni la kidunia zaidi, wananchi wako sahihi kudai, hivyo NEC iliitaka serikali kutekeleza sera na mikakati ya kupunguza makali ya matatizo hayo," alisema.

Tatizo jingine alilozungumzia ni rushwa kwenye huduma za wananchi ambapo alisema wananchi wengi wamekuwa wakilalamikia rushwa hospitalini, mahakamani, ofisi za ardhi, polisi, shuleni na kwenye ajira na kwa kuwa watendaji katika maeneo haya ni wa serikali ya CCM, wananchi wanalalamikia serikali ya CCM na chama chenyewe kama chanzo cha rushwa hii kutokana na kushindwa kudhibiti, hivyo katika hili alisema NEC iliitaka serikali kuchukua hatua za makusudi kuondoa kero ya rushwa.

Kutokana na hali hiyo, aliwataka wana-CCM hao kutafakari kila mmoja na kujipanga upya ili kuimarisha chama hicho na kuondokana na madoa yaliyopo kwa sasa na hii alisema inatokana na CCM kutozoea ushindi mwembamba ambao ulitoka asilimia 80 mwaka 2005 hadi asilimia 60 mwaka jana.

"Kama kuna matatizo tuyashughulikie kwa umakini na hasa katika tuhuma za rushwa na ufisadi...tushughulikie watuhumiwa wa kweli bila kuoneana aibu wala kuonea watu wengine ili vita hii iwe na tija kwani huwezi ukasema kuwa fulani ndo amekikosesha ushindi chama na wakati jimboni kwake kashinda kwa asilimia zaidi ya 80...katika hili tuwe waungwana tusimamie ukweli," alisema.

2 comments:

  1. akhsante Mahanga umesema kweli. Naongeza kwa kutahadharisha kwamba huu mpango mpya wa kuanzisha matabaka kwenye ada ya uanachama unaweza kuua juhudi zote za mwenyekiti kujenga chama chenye usawa. Tuwe makini kwenye maamuzi. Hii ni hatari.

    ReplyDelete
  2. Hapa nimethibitisha kuwa Mhe. PhD yako si ya Kifisadi maana umetoa point tupu. Mimi namshangaa Nape kwa jinsi anavyoitafsri dhana hii ya kujivua gamba iwe ya kulipizana visasi. Kasi yake ni nzuri lakini ni hatari kwa CCM na sijui Nape anauelewa kiasi gani. Kama CCM mnajua mna katibu mwenezi hapa nawaambia mmeula wa chuya. Ni jina tu la Nnauye ndilo linamsaisia. Namfahamu Marehemu Mzee Nnauye (Mungu amrehemu) kama angekuwa hai asingekubali mhuni huyu kupewa wadhifa mkubwa namna hii. Nawatahadharisha CCM hivi barua hizo wanazoaandaa zinakwenda kwa akina nani? Na hao ni mahakama ipi imewahukumu? Kama Nape na sekretarieti yake watatumia orodha ya Dr. Slaa, humo pia hata mweyekiti wao ametajwa, je Nape ameandaa barua kwa mwenyekiti wake Rais kikwete?. Hapa ni tatizo, kama watu weledi pekee kama akina Dr. Mahanga wanaona ni kuna tatizo basi kuna haja ya wazee kumkanya Nape asipende sana kuropoka. Nafahamu vizuri na tangu aanze kutawala nimeanza kumwelew rais kikwete hawezi kumtuma Nape aongee ujinga hata Kidogo. kama anafurahishwa na upuuzi wa Nape basi nae anatatizo. Nape hacelei kusema kila mwenye kuhoji kuhusu kujivua gamba basi anaatetea mafisadi. Lakini Nape hawataji mafisadi ni akina nani? Tunaambiwa huko ndani ya vikao vya CCM walitajwa Chenge, Rostam na Lowassa, lakini CCM haijaweka wazi maana hizo ni mbwembwe za magazeti. Angalieni kijana huyu anaipeleka CCM shimoni anaivisha gamba lingine baada ya kulivua.

    ReplyDelete