23 May 2011

Madiwani waijia juu serikali, wabunge

Na Mwandishi Wetu

KAULI ya Mbunge wa Kwela, Bw. Aloyce Molocha iliyoonesha kuwakejeli madiwani imeibua 'mambo' baada ya madiwani wa Manispaa ya Kinondoni kuibuka wakisem
a kuwa amani ya nchi iko mashakani kwani wananchi kukabiliwa na njaa inayotokana na ugumu wa gharama za maisha kutokana na serikali kushindwa kuwajibika ipasavyo.

Baadhi ya madiwani hao wamelalamikia kauli ya mbunge huyo, ambaye hivi karibuni katika taarifa ya habari ya moja ya kituo cha runinga nchini, alisikika akisema kuwa diwani hana uwezo wa kuzungumza na waziri wala rais, hivyo anayeweza kutatua matatizo ya wananchi na kuwasemea ni mbunge.

Wakionekana kukerwa na kauli mbalimbali zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali walizodai kuwa zinawadhalilisha mbele ya watu, madiwani hao wamesema kuwa sasa wameishiwa na uvumilivu, wako tayari kupambana na mbunge au kiongozi yeyote anayetoa kauli za 'kuwadogodesha' kwani wao ndiyo wako na wananchi.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, wakiwa katika kamati ya jumla ya madiwani, baadhi ya madiwani walisema kuwa uvumilivu wao ndiyo unaowafanya wadharaulike wakati wao ni wawakilishi halali katika ngazi ya serikali za mitaa iliyopo kwa mujibu wa sheria, hivyo wamemtaka Waziri Mkuu Mizengo Pinda kutoa kauli yake.

Diwani wa Kata ya Magomeni, Julian Bujugo alisema kuwa kamati hiyo ilikutana na waandishi wa habari kwa ajili ya kuzungumzia mambo mbalimbali kwa ajili ya kujenga mustakabli wa nchi.

"Tunachosema hapa ni kwamba tustiriane. Hata sisi tunajua mambo yao mengi tu...yako mambo mengi tu ya wabunge tukitaka kuyazungumza yatapoteza heshima yao...Kwa mfano juzi walitaka kupigana bungeni kwa suala la ajabu lakini sisi hatujasema kitu. Kwa muda mfupi tangu waingie bungeni wameitumbukiza nchi gizani.

"Kweli kwa busara zao wanakubali nchi iingie iwe gizani wananchi tuteseke sababu ya mikataba mibovu, kwani mikataba mibovu ni nini...sisi tunawastili ndugu zetu hawa. Lakini sasa tumechoshwa, hii dharau ya wabunge kwa madiwani tumeivumilia muda mrefu sasa, uvumilivu wetu ndiyo chanzo cha kudharauliwa.

"Tunadharauliwa wakati tunapata posho ya laki moja na elfu ishirini kwa mwezi, pesa ndogo kabisa tunazidiwa hata na ma-house girl au ma-house men, au bar maid...wenzetu wananufaika tu...mbunge anapata mkopo mpaka wa sh milioni mia mbili CRDB, anapata mkopo wa gari milioni 90, bado anajipatia mshahara mkubwa," alisema Bw. Bujugo.

Mbali na hilo, diwani huyo aliongeza kuwa nchi sasa inaendeshwa bila ya mipango ya uhakika kuondoa tatizo la ajira na vijana wa mitaani, akishauri kuwepo kwa mikakati madhubuti kuwasaidia kuendesha maisha yao pia wazalishe kwa ajili ya taifa kama ilivyokuwa enzi za 'Mwalimu' ambapo vijana walikuwa wakitumika kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).

Alisema hakuna mikakati ya kuhakikisha nchi inakuwa na viwanda vidogo vidogo, kushughulikia hali ngumu ya gharama za maisha inayowakabili Watanzania wengi kwa sasa, akihoji 'nani anaweza kula mlo mmoja kwa sh elfu tano kwa wananchi wa kawaida, ambapo unga unauzwa sh. mia nane kwa kilo.

"Sasa hivi watu wengi wanakabiliwa na njaa, ni aibu kwa taifa kama Tanzania watu wake kukabiliwa na njaa...hii itasababisha na kuzua matatizo na vurugu baadaye, kwani mwananchi wa kawaida hatakubali kumuona mbunge akipita na gari lake wakati yeye hana uhakika wa kula.

"Serikali inatakiwa kujenga uchumi wa nchi kila mtu aweze kujilisha yeye na familia yake...nchi sasa hivi inakwenda bila mipango, rais anawapeleka darasani kila mara lakini hakuna kitu, utafikiri nchi haina wataalam...hawafundishiki awatoe, atupatie sisi madiwani tuendeshe nchi," alisema Bw. Bujugo.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Makurumla, Bw. Rajab Hassan alisema kuwa kauli hizo kama ya Mbunge wa Kwela, juu ya 'kuwadogodesha' madiwani, zinawadhalilisha, akisema ni bora 'wakaheshimiana' sasa.

"Mbunge wa Kwela, amesikika akisema mbele ya wananchi kuwa diwani hana uwezo wa kuzungumza na waziri, hana uwezo wa kuzungumza na rais. Huu ni udhalilishaji mkubwa, hawa wote wamechaguliwa na wananchi, wote wanawatumikia wananchi. Kama diwani hana uwezo wa kuzungumza nao sasa wananchi wanasemewa na nani...tuheshimiane," alisema Bw. Hassan.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Sinza, Bw. Renatus Pamba, alisema kuwa kutokana na kauli yake hiyo dhidi ya madiwani, Bw. Molocha ameidhalilisha ofisi ya waziri mkuu ambayo ndiyo inahusika kusimamia serikali za mitaa kupitia Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

"Lazima wabunge watambue kuwa madiwani wana kazi kubwa sana. Local government (serikali ya mtaa) ndiyo msingi na zimewekwa kwa mujibu wa sheria...hatuwezi kumuelewa mtu wa namna hiyo. Kwanza amedhalilisha hata Ofisi ya Waziri Mkuu. Watambue uwepo wa serikali hiyo," alisema Bw. Pamba.

Naye Diwani wa Kunduchi, Bi. Janeth Rithe, alisema 'kauli hizi zinaonesha kuwa wabunge hawako tayari kutusaidia...tunataka wabunge wenzake wamuonye na aombe radhi...hii dharau sasa imefika pabaya...sisi ndiyo tuna watu wao hawana watu," alisema Bi. Rithe.

Chanzo cha kauli ya Bw. Molocha, ambaye aliitoa katika Kijiji cha Lusaka pamoja masuala mengine, ni kufungwa kwa shule ya sekondari ya kata katika eneo hilo, ambayo hivi karibuni wananchi wake walilalamika mbele ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kuwa imefungwa kwa sababu ta itikadi za kisiasa.

Wakitoa madai yao mbele ya wabunge hao, Bw. Kabwe Zitto, Bi. Joyce Mkya na Bi. Raaya Ibrahim, wananchi wa Lusaka walisema kuwa shule hiyo ya sekondari iliyo pekee katika maeneo yao, ilifungwa bila maelezo yoyote ya msingi, lakini wao wanajua imefungwa kwa sababu walichagua diwani wa CHADEMA.

Walidai kuwa ilifungwa na viongozi wa serikali Manispaa ya Sumbawanga, takribani miezi mitatau iliyopita bila kuwashirikisha wao kujua sababu za msingi.

2 comments:

  1. asante, yote ni magamba yanaendelea kupukutika...hamjui tanzania inajengwa na wenye moyo na kuliwa na wenye meno?

    ReplyDelete
  2. magamba ondokeni ,na ccm iondoke pia

    ReplyDelete