Na Grace Michael
RAIS Jakaya Kikwete ametakiwa kuueleza umma hatua ambazo serikali yake inakusudia kuchukua kurekebisha matatizo yanayoikumba sekta ya umeme ikiwemo
kuwachukulia hatua wote waliohusika au kushindwa kuwajibika ipasavyo kumaliza tatizo hilo.
Mbali na hilo, Waziri wa Nishati na Madini Bw. William Ngeleja naye ametakiwa kuwajibika kutokana na athari za kutochukua hatua haraka hali inayosababisha kuendelea kuwepo kwa mgawo wa umeme.
Tamko hilo limetolewa jana na Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, Bw. John Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Ubungo kupitia chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).
“Rais akiwa ndiye Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri anatakiwa kueleza kwa umma hatua ambazo serikali yake inakusudia kuchukua kurekebisha hali hiyo kwani
alishatembelea wizara na kutoa maagizo na akarudia tena maagizo yale yale kwa kutumia mamilioni ya walipa kodi kupitia semina elekezi, kinachotakiwa hivi sasa
sio maagizo tena bali ni mkuu wa nchi kuchukua hatua,” alisema Bw. Mnyika.
Alisema kuwa endapo tamko hilo halitazingatia maelezo na vielelezo zaidi vitawasilishwa kwenye vikao vya kambi rasmi ya upinzani na hatimaye masuala husika na mengine zaidi kuibuliwa bungeni kwa ajili ya wahusika kuwajibishwa.
Katika tamko hilo, Bw. Mnyika alieleza kuhusu mgawo wa umeme unaotokana na upungufu wa gesi ambapo alisema kuwa hali hiyo imetokana na mamlaka husika
kutokuwajibika ipasavyo.
Alisema kuwa matengenezo ya mitambo hiyo yalifahamika kwa serikali kuanzia mwishoni mwa mwaka 2010 na Februari 2011 na kujadiliwa ndani ya serikali.
“Kuna tuhuma za muda mrefu kuwa Kampuni ya Pan African imekuwa haifanyi matengenezo ya ukamilifu na kwa wakati hata hivyo wizara inayohusika haikueleza
hatua ambazo zimechukuliwa hali ambayo imeongeza hitaji la matengenezo makubwa kwa wakati mmoja yaliyosababisha gesi kutokusambazwa na kuleta upungufu wa umeme wa kati ya Megawati 200 mpaka 359 katika kipindi husika lakini serikali haijachukua hatua za haraka kumaliza tatizo hilo,” alisema Bw. Mnyika.
Alisema kuwa hali ya utegemezi wa serikali kwenye sekta ya gesi kwa kampuni yenye mwelekeo wa udalali imesababisha hasara na ina mwelekeo pia wa kuhatarisha
usalama wa nchi katika siku za usoni kama hatua stahili hazitachukuliwa
Hivyo Bw Mnyika aliiomba Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuchunguza hali hiyo na
kuchukua hatua mapema.
“Serikali inapaswa kupitia upya mikataba na kampuni ya Songas, Pan African na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) ili kuondoa migongano na kupunguza mzigo
kwa taifa wakati gesi asilia ni mali asili ya Watanzania sambamba na kupanua wigo wa usafirishaji wa gesi katika mwaka wa fedha 2011/2012,” alisema.
Alisema suala lingine ambalo alizungumzia ni hatua za dharura za kupunguza upungufu wa umeme ambapo alitahadharisha kwamba mgawo mkubwa na wa muda mrefu utalikumba taifa kuanzia Julai mwaka huu kutokana na hatua za dharura kutochukuliwa kwa wakati.
Alisema pamoja na serikali kushikilia msimamo wa kukodi mitambo ya umeme wa Megawtai 260 ambayo itatumika kwa kipindi cha miezi sita pekee kwa gharama za zaidi ya bilioni 400 badala ya kuweka mkazo katika kununua mitambo kama ambavyo imeshauriwa na wadau mbalimbali, Wizara ya Nishati na Madini haijawajibika kwa kiasi cha kutosha kuhakikisha nchi haikumbwi na mgawo.
Bw. Mnyika alisema kuwa mchakato wa kutekeleza mpango wa dharura umecheleweshwa na hivyo kuna hatari ya mitambo hiyo kuwa tayari kutoa huduma mwezi Januari
katika kipindi ambacho haihitajiki na kusababisha hasara kwa taifa kama ilivyokuwa kwa mitambo ya Richmond.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali inapaswa kusitisha mara moja mpango huo na kuelekeza fedha hizo za umma katika hatua za dharura za kununua mitambo ya
kudumu na kinyume na hapo itathibitika kwamba kuna mazingira ya ufisadi katika mpango huo wenye kutaka kuongeza mzigo wa madeni kwa TANESCO na gharama za umeme kwa wananchi wa kawaida.
Alisema kuwa madhara na hasara yote ambayo wananchi, sekta binafsi na serikali imekuwa ikipata kuanzia Februari mwaka mwaka huu mpaka Desemba 2012
inatokana na kutokuwajibika kikamilifu kwa mamlaka husika kwa kuwa dharura ilifahamika tangu 2008
Alisema kuwa serikali ikapanga kwamba utekelezaji wa miradi ikiwemo ya kutumia mafuta mazito Mwanza na Mradi wa kutumia gesi asilia Ubungo, Kiwira ilipaswa kukamilika Februari mwaka huu lakini kutokana na uzembe, ufisadi miradi hiyo itakamilika 2012/2013.
Suala lingine alilozungumzia ni tuhuma za ufisadi katika manunuzi kwa ajili ya miradi ya umeme ambapo aliweka wazi kuwa serikali haijawajibika ipasavyo
kushughulikia tuhuma za ufisadi katika ununuzi wa mafuta mazito ambayo Waziri wa Nishati na Madini alieleza bungeni Aprili kwamba zimetumika sh. bilioni 46 kwa ajili ya kuendesha mitambo ya kufua umeme ya IPTL ambapo Mei, mwaka huu.
Alisema kuwa Wizara ya Nishati na Madini kupitia taarifa nyingine ilisema kwamba fedha zilizotumika kwenye ununuzi wa mafuta katika kipindi husika ni sh. bilioni 28 bila kueleza sababu za kutofautiana kwa maelezo ya waziri bungeni na haya yaliyotolewa.
Alisema kuwa kutokana na hali hiyo, Kamati ya Nishati na Madini inapaswa kufanya uchunguzi maalum kama ilivyoombwa na Mwenyekiti wa Kamati za Hesabu za Mashirika ya Umma, Bw.Zitto Kabwe.
Awabane vipi ilhali yeye ndio mhusika mkuu?Kwani IPTL ilikuja wakati gani?N Richmond,Dowans je?
ReplyDelete