02 May 2011

TUCTA yataja mbinu kuongeza mishahara

*Mgaya ataka misamaha ya kodi, posho za vigogo zipunguzwe
*Ataja matumizi makubwa ya serikali, safari za viongozi
*Kikwete aahidi kuangalia uwezekano kuongeza kima cha chini


Na Ramadhan Libenanga, Morogoro

SHIRIKISHO la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) limeitaka serikali kupunguza
misahama ya kodi, posho na kupunguza tofauti ya mshahara wa kima cha chini na mshahara wa juu ili uweze kumudu kulipa mashahara wenye tija kwa wafanyakazi.

Hayo yalisemwa na Kaimu Katibu Mkuu wa TUCTA, Bw. Nicholaus Mgaya alipokuwa akisoma risala ya shirikisho la vyama vya wafanyakazi Tanzania mbele ya Rais Kikwete katika sherehe za Mei Mosi mkoani Morogoro jana.

Bw. Mgaya alisema kuwa serikali inao uwezo wa kulipa kima cha chini cha mshahara utakaoweza kukidhi mahitaji ya msingi ya maisha ilimradi uwepo utayari wa kukubali kutekeleza ushauri unaotolewa na shirikisho hilo.

Alisema kuwa TUCTA imebaini kuwa washauri na watendaji wa serikali  wanatumia hoja za kuifanya serikali ionekane kujitetea zaidi hata kwa ushauri wa wazi usiohitaji malumbano.

Bw. Mgaya alisema kuwa TUCTA inapenda tena kuishauri serikali kwa mara  nyingine kuwa, inapaswa kupunguza misamaha ya kodi hadi asilimia 1 ya pato la taifa, hatua ambayo itaokoa zaidi ya sh. bil. 600 kila mwaka.

Alisema kuwa taarifa zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 53 ya misamaha ya kodi yote inayotolewa nchini hunufaisha zaidi kampuni kubwa za biashara ya kimataifa zinazowekeza katika sekta ya madini, viwanda na biashara.

“Serikali ipunguze misamaha ya kodi kama inavyofanyika katika nchini nyingine za Afrika Mashariki,” alisema Mgaya.

Ushauri mwingine kwa serikali kutoka TUCTA, ni kwamba posho ya mishahara  halisi isijumuishwe katika fungu moja la bajeti ya mishahara kwa sababu posho hawazipati watumishi wote wa umma.

Alidai kuwa posho hizo zinalipwa zaidi kwa watumishi wa umma wa ngazi ya juu tu, kwenye wizara ambao ni asilimia 30 tu ya watumishi wote wa umma, hivyo posho hizo zimekuwa zikipotosha ukweli.

Ushauri mwingine ni pamoja na kupunguza tofauti ya mshahara wa kima cha  chini na mshahara wa juu, wigo wa walipa kodi upanuliwe na ukwepaji kodi udhibitiwe.

Pia shirikisho hilo liliitaka serikali kupunguza matumizi yasiyo ya lazima na kuzuia upotevu wa fedha za umma, hatua ambayo ingeweza kuokoa fedha nyingi za serikali ili zielekezwe kutatua matatizo mengine ikiwemo mishahara ya wafanyakazi.

Alibainisha kuwa matumizi ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele ni pamoja na malipo ya posho zisizo za lazima, gharama kubwa za semina, misafara mikubwa ya viongozi ndani na nje ya nchi, ununuzi wa mafuta na matengenezo ya magari ya serikali na gaharama kubwa za makaribisho (hospitality).

Katibu mkuu huyo wa TUCTA alisema kuwa kama serikali ikizingatia ushauri huo na kutekeleza, itafanikiwa kuokoa mabilioni ya fedha ambazo zilikuwa zikitumika pasipo na maslahi ya taifa na zikiinmgizwa katika bajeti ijayo ya mwaka 20011/2012 kuboresha mishahara ya wafanyakazi, kuwapunguzia mzigo wa kodi ya mapato (PAYE) na kuboresha pensheni ya wastaafu.

Akiwahutubia wafanyakazi hao na taifa kwa ujumla, Rais Kikwete alisema kuwa serikali inatambua madai ya wafanyakazi nchini, kuwa ni madai ya msingi lakini bado ipo katika mchakato wa utekelezaji wa madai ya wafanyakazi nchini.

Alisema kuwa kutokana na ufinyu wa bajeti serikali bado ipo katika mchakato wa kutatua kero hizo kwa awamu.

"Ahadi ninayopenda kurudia tena leo ni kuwa tutaiendeleza kazi tuliyoianza mwaka hadi mwaka.  Hata hivi sasa katika mchakato unaoendelea wa kutayarisha bajeti ya mwaka ujao wa fedha, wahusika wanaangalia namna ya kupandisha kima cha chini cha mashahara na nafuu nyinginezo.

"Risala yenu imejitosheleza kwa hoja na ina ushauri mwingi mzuri kuhusu mikakati ya kuboresha mishahara na maslahi ya wafanyakazi. Napenda kuwahakikishia kuwa tumeupokea kwa mikono miwili ushauri huo na tutaufanyia kazi.

"Nakubaliana na ujumbe wa kaulimbiu yenu ya mwaka huu kwamba “Serikali isipojali haki zenu, wafanyakazi watakuwa watumwa ndani ya nchi yao”.  Ni ukweli uliowazi kwamba serikali inao wajibu wa kulinda haki za wafanyakazi nchini. Lakini ni kweli pia kwamba wajibu wa kulinda haki za wafanyakazi hauko mikononi mwa serikali pekee.

"Upo pia kwa waajiri na wafanyakazi wenyewe kupitia au kwa kuongozwa na vyama vyao.  Mimi naamini, wote tukitimiza wajibu wetu ipasavyo, tutaweza kuyapatia ufumbuzi matatizo yanayowakabili wafanyakazi hapa nchini

Aliwataka waajiri nchini kuacha kukwepa majukumu yao kwa mujibu wa sheria ya kazi nchini na badala yake kufuata maadili ya kazi na sheria zake.

Rais Kikwete alisema kuwa kumekuwa na wimbi kubwa la waajiri kukiuka kwa maksudi sheria za kazi kwa lengo la kukwepa majukumu yao yaliyopo kwa mujibu wa sheria ya kazi.

“Ni kosa la jinai kwa mwajiri kuvunja sheria ya kazi kwa makusudi, hivyo naviomba vyombo vya sheria nchini kuwachukulia hatua kali waajiri wote wanaovunja sheria za kazi," alisema Rais Kikwete.

4 comments:

  1. Maandamana na migomo ndio njia nzuri ya kuionyesha serikali isivyowajali wafanyakazi.
    RISALA NI NZURI KILA MWAKA NI HIYO TU,Utelezaji wake mbona sifuli?TUKTA
    Kukutana na Rais sio ujiko nyie kazi yenu ni kutetea wafanyakazi na RAIS yeye mwenyewe anamatumizi makubwa na mawaziri mabosi wa wizara 30% jamani watu wanapata posho kuliko mshahara hivi hiyo ni haki kwa mfanyakazi wa kima cha chini ni KUUA WANANCHI WENGI WANATEGEMEA WAFANYAKAZI

    ReplyDelete
  2. angalia nchi za ulaya na merica first priority ni watumishi , wanapewa mikopo ya nyumba magari na mishahara minono.hapa mikopo wanapewa wabunge tu angalia magari wanayotembelea wabunge gari moja inajenga zahanati tano leo mnasema hamna hela , mishahara ya wabune na posho zao nihela nyingi sana serikali inawalipa tu bila taabu leo iweje watumishi wasilipwe pesa nzuri ?malipo ya wabunge na mawaziri yanatoka wapi , africa hatujali watu wetu tuna ubinafsi na uroho , hakuna mbunge wala aziri anayetetea haki za wananchi . bado hatuna kiongozi mwenye uchungu na watu wake alikuwa nyerere peke yake, hivi mimi nauliza unaweza kwenda kuwekeza ulaya ukapewa msamaha wa kodi ? na wasipo turekebishia mambo yetu hatuwapi kura tena

    ReplyDelete
  3. Kwa hili napenda kwa dhamira ya kweli nimpongeze Rais kwa kukubali kuwa wafanyakazi tunapata mishahara kiduchu ilhali gharama za maisha zimepanda. Hata kama wengine watakuwa hawataki lakini ni ukweli usiofichika kuwa serikali imejivua gamba la kutokuwa sikivu na sasa ina sikia. Kwa Rais kukubali na kuagiza mishahara ipandishwe ni hatua nzuri lakini ninawasiwasi na watendaji hasa Waziri Hawa Ghasia na maofisa wake katika wizara ya utumishi wa Umma. Badhi ya Waajiri hasa wakurugenzi na maafisa utumishi katika Halmashauriza wilaya ni wanyanyasaji wa kutupwa. Pamoja na kuwa mhe. Mgaya kueleza yanayojitosheleza kwa Rais Kikwete mimi pia kama mtumishi wa Halmashauri naomba nijazilize pale ambapo Mgaya amebakisha. Hii ni kutokana na dhamira nzuri ya Rais kikwete ya kutaka maslahi bora kwa wafanyakazi wake. Kama mhe. Rais au wasaidizi wake wanasoma safu hii basi naomba wazichukue hoja zangu kwa umakini mkubwa na wazifanyie uchunguzi waone ukweli uko wapi.
    Nina hoja nyingi lakini leo nieleze moja tu:
    Tofauti ya mishahara kati ya maafisa wa ngazi za juu na wale wa ngazi za chini.
    Mheshimiwa Rais, Hili ni tatizo na ndilo linasababisha wafanyakazi kukata tamaa na kuwaachia kundi hili la wateule wa Rais wafanye kazi wao. Wakati naanza kazi katika Halmashauri mwaka 1998 mimi nilikuwa na stashahada katika fani yangu wakati mkuu wangu wa idara akiwa na stashada ya juu/shahada ya kwanza katika fani hiyohiyo, nilikuwa napata mshahara wa shs.45,000/= na yeye akipata 90,000/= hivi. Lakini leo hii mimi nina shahada ya kwanza na mkuu wangu huyo nae anashahada lakini mimi napata 400,000/= na yeye anapata Shs. 1,700,000/=.Tulipojaribu kuhoji tukaambiwa huo ni mshahara wa madaraka. Sasa hebu angalia, kwenye Halmashauri wafanyakazi wanaotambuliwa na serikali yako ni hawa maana hao ndio pamoja na mishahara yao mikubwa wanapata posho za semina ni wao, kusafiri nje ya kituo ni wao, kila kitu chenye maslahi ni wao. Huko wilayani tuliko pamoja na madaraka yao hayo lakini tunaenda soko moja, wote tuna watoto wanaoenda shule na mahitaji ya msingi kwa wote ni sawa. Tofauti ni kuwa wenzetu hawa wana magari ya kifahari na wamejenga majumba ya kifahari huku wakiishi bure kwenye nyumba za serikali huku sisi tukiumia kwa kulipa kodi ya pango. Hili linazaa dharau na makundi miongoni mwa wafanyakazi wa Halmashauri za serikali za mitaa. Watumishi wengine ambao wana shule nzuri lakini si wakuu wa idara wamekuwa wakiacha kazi na kutafuta maslahi kulingana na elimu yao mahali pengine baada ya pengine kusomeshwa na serikali kwa gharama kubwa. Usemi wa kiswahili usemao "aliyeshiba hamjui mwenye njaa" umekuwa ukijidhihirisha maana katika hili sijawahi kusikia mkuu wa idara au mkurugenzi ambae ni mwajiri akidhubutu kutetea hili. Wakati fulani naibu katibu mkuu wa Tamisemi alitembelea Halmashauri ambayo mimi nafanya kazi. Tulipojaribu kumwomba aliangalie hili kuwa ni tatizo, tuliambulia matusi na kejeli kuwa tunataka kufanana na mabosi wetu. Zaidi naibu KM huyu kijana aliishia kujisifia yeye akidai kuwa Mheshimiwa Rais amemwona akiwa bado kijana wa miaka 45 na hakuna hata moja alilojibu kwa manufaa ya wafanyakazi waliomuuliza maswali.
    Mhe. Rais suala hili upishano mkubwa wa mishahara si suala la kufanyia mchezo maana hakika nakwambia linashusha ari na moyo wa kufanya kazi kwa wafanyakazi wa ngazi ya kati na wa chini ambao ndio wafanyaji wa kazi na waleta taarifa kwa hawa mabosi wanaopewa mvua ya mishahara. Badala yake linazalisha matabaka kati ya mabwana na watwana katika serikali za mitaa. Mimi nimejitolea na niko tayari hata kwa kufukuzwa kazi lakini hili nitamuandikia Mheshimiwa Rais kumweleza wazi na kutokana na utafiti niliofanya. Kwa kuwa nafasi ni finyu ushauri ninaotoa ni kuwa kama serikali itaendelea kuwapendelea hawa wateule wake basi na wafanyakazi wengine walipwe kulingana na majukumu yao na uzito wa kazi wanazozifanya kitaaluma. Kama hilo haliwezekani basi mishahara ya hawa wateule isimame hapo na serikali iboreshe hawa wa chini walau tofauti isiwe kubwa kiasi hiki.

    ReplyDelete
  4. Kupandisha mishahara sawa. Shida iliyopo ni kwa kiasi gani. Mimi sijali sana suala la ukubwa wa tarakimu za mishahara. Maana hata ikipandishwa hadi kufikia kima cha chini 1,500,000, Je mfumuko wa bei utakuaje. Ukitafsiri kupanda kwa mishahara kwa kuangalia tarakimu, hapa tutakuwa tunadanganyana. Hebu tuchukulie mfano Serikali ikaacha kupandisha mishahara mwaka huu, halafu badala yake ikashusha kodi katika nishati (mafuta na umeme) kwa asilimia 50%, na pia Serikali ikaendelea na utaratibu wa kununua vyakula kwa wakulima na kusambaza kama ilivyoanza sasa kwa upande wa mahindi ambayo punde tunaanza kununua unga kwa shilingi mia 500 badala ya 1,000 ya sasa. Mbinu ya aina hii ya kiuchumi ingesaidia sana kuona thamani ya mishahara iliyopo sasa kuliko kukazania kuongeza tarakimu.
    Serikali ipunguze kodi kwenye nishati, Serikali ibuni vyanzo vipya vya mapato ambavyo vingi vimedumaa au kuachwa hivihivi na pia Serikali iboreshe usimamizi wa matumizi yake, nk.

    ReplyDelete