17 May 2011

Kocha Chelsea aaga mashabiki

LONDON, Uingereza

CARLO Ancelotti 'amewaaga' mashabiki wa Chelsea na kusema kuwa hajui kama ataendelea kuwepo katika klabu hiyo kwenye msimu ujao.Kocha huyo jana alishuhudia
timu yake ikibanwa na kutoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Newcastle, katika mechi yao ya mwisho ya nyumbani.

Ancelotti alisema: "Sijui ni kitu gani kitatokea. Hakuna mkutano uliopagwa lakini tutalazimika kusubiri kwa wiki moja tu.

"Kila mmoja anaweza kuwa na mawazo yake kuhusu kazi yangu, lakini ni klabu inayoamua hatima yangu na kufanya maamuzi.

"Kama kazi ilikuwa nzuri, nitabakia. Kama wanafikiri haikuwa nzuri, nitaondoka.

Kwa mawazo yangu, ninaona wakati mwingine nimefanya kazi nzuri na wakati mwingine ninaweza kufanya vizuri."

Ancelotti aliongeza: "Kwanza kabisa ninataka kuwapongeza mashabiki wetu. Wameniunga mkono kwa hali ya kusisimua katika msimu wote."

Mmiliki wa timu hiyo, Roman Abramovich jana alishuhudia timu yake ikipoteza pointi mbili baada ya wapinzani wao Newcastle United kusawazisha bao la pili katika muda wa majeruhi.

Ancelotti aliongeza: "Wakati unaporuhusu kufungwa magoli mengi dakika ya mwisho, si kitu."

Katika mechi nyingine zilizochezwa jana, Wigan ilikamilisha safari ya kushuka daraja ya West Ham, baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2. Bao la ushindi la Wigan lilifunga katika muda wa majeruhi na Charles N'Zogbia, likiwa ni goli lake la pili katika mechi hiyo.

Wigan sasa iko sawa kwa pointi 39 na Birmingham, huku ikiwa imesaliwa na mechi moja.

Arsenal ilifungwa mabao 2-1 na Aston Villa, nayo Birmingham ilifungwa mabao 2-0 dhidi ya Fulham na Liverpool ikiwa nyumbani ilichapwa mabao 2-0 na Tottenham, ambayo sasa imekuwa nafasi ya tano na Liverpool kushuka nafasi ya sita.

No comments:

Post a Comment