17 May 2011

Bingwa wa Olimpiki Kenya afariki

NAIROBI, Kenya

BINGWA wa Olympiki katika mbio za masafa marefu za Marathon Mkenya, Samuel Wanjiru ameaga Dunia kwa kile kinachosemekana kwamba amejiua.Duru za polisi
zinasema, Wanjiru alikumbana na mauti hayo baada ya kuruka kutoka chumba chake cha ghorofa moja katika eneo la Nyahururu, Mkoa wa Kati wa Kenya.

Idara ya polisi imethibitisha kifo hicho na kusema kwamba uchunguzi umeanza, ili kubainisha sababu za kifo hicho.

Mwanariadha huyo alishinda medali ya dhahabu katika mbio za Olimpiki mwaka wa 2008 mjini Beijing, kwa kukimbia kwa muda wa saa 2:06:32 na kuweka rekodi ya kuwa Mkenya wa kwanza kushinda mbio za marathon kwa upande wa wanaume.

Wanjiru pia alikuwa bingwa wa Dunia katika misururu ya mbio za marathon, maarufu kama World Marathon Majors kuanzia mwaka wa 2008 hadi mwaka wa 2010.

Wanjiru pia aliweka rekodi ya mbio za kilometa 21 kwa kuandikisha muda wa dakika 58:33.

Decemba mwaka jana, Wanjiru alifikishwa mahakamani, kwa mashtaka ya kutishia kumuua mkewe, kumjeruhi mlinzi wake wa nyumbani na pia kumiliki bunduki aina ya AK-47 bila idhini ya serikali.

Mapema mwaka huu, Wanjiru alihusika kwenye ajali mbaya ya barabarani akiwa anatoka Nairobi kwenda Nyahururu, hatua iliyomfanya kujiondoa mbio za London Marathon.

No comments:

Post a Comment