Na Zahoro Mlanzi
KAMBI ya timu ya Taifa 'Taifa Stars', iliyotakiwa ianze jana, imesogezwa mbele mpaka Mei 7, mwaka huu jijini Dar es Salaam.Timu hiyo inajiandaa na mchezo wa
kirafiki wa kimataifa utakaopigwa mwishoni mwa mwezi huu dhidi ya Afrika Kusini 'Bafana Bafana'.
Mbali na mchezo huo, Taifa Stars pia itaumana na Jamhuri ya Afrika Kati katika mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika, utakaopigwa Juni 4, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, alisema Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jan Poulsen, ndiye aliyeamua isogezwe mbele.
Alisema kutokana na programu ya kocha huyo ya kujiandaa na michezo hiyo miwili aliyoiwasilisha TFF, ndiyo iliyoeleza mambo hayo.
"Kocha amewasilisha programu yake na inaonesha timu hiyo itaingia kambini Jumamosi, badala ya leo (jana), hivyo tumewataarifu wachezaji juu ya jambo hilo," alisema Wambura.
Alisema mawasiliano na Afrika Kusini yanaendelea na kikubwa wanachokisubiri ni kupanga tarehe ya kucheza mchezo huo na siku watakayotua nchini.
Alisema kikosi kitakachoingia kambini ni kile kile kilichokwenda nchini Msumbuji kucheza na timu ya taifa ya nchi hiyo, na labda waongezeke wanaocheza soka la kulipwa.
No comments:
Post a Comment