03 May 2011

Matumla atetea mkanda wake

Addolph Bruno

BONDIA wa ngumi za kulipwa nchini, Mbwana Matumla,  amefanikiwa kutetea ubingwa wake wa mabara wa UBO Intercontinental kwa kumchapa Mkenya Gabriel Ochieng kwa
pointi, katika pambano lililofanyika ukumbi wa PTA Sabasaba jijini Dar es Salaam, juzi.

Pambano hilo lilikuwa ni la raundi 12, uzani wa bantam kg 53.3, liliandaliwa na Leonidas Kabanga na kusimamiwa na Shirikisho la Ngumi za kulipwa Tanzania (PST) chini ya Rais wake, Emanueli Mlundwa lilichezeshwa na mwamuzi Anthon Ruta.

Pambano hilo lilianza kwa mabondia wote kuonesha umahiri katika raundi ya kwanza mpaka ya saba, lakini Matumla alionesha umahiri wake zaidi katika raundi ya nane kwa kumwangushia mpinzani wake makonde mazito.

Katika raundi ya 10, Matumla alimrushia makonde mfululizo mpinzani wake yaliyomdondosha chini, lakini aliendelea mpaka raundi ya mwisho na baadae majaji wa mchezo huo wakatoa ushindi kwa Matumla.

Jaji wa kwanza Billy Kiremi alitoa pointi 120 – 117 , Hassan Mwingira pointi 120 – 114 , na Jalus Ligongo pointi 116 - 113.

Pambano hilo lilitanguliwa na mengine ya utangulizi, ambapo Shabani Mtengela alishinda kwa TKO katika raundi ya kwanza dhidi ya Idrisa Issa, ambao walicheza uzani wa feather raundi ya nne.

Bondia Sadiki Momba alitoka sare na Jumanne Mpombe, baada ya kugongana vichwa kwa bahati mbaya katika raundi ya kwanza, hali iliyomsababishia Sadiki kupata maumivu makali katika pambano hilo la uzani wa feather,  huku Fadhili Majia akimchapa kwa TKO raundi ya pili Kijepa Omari, pambano lao lilikuwa la raundi nne.

Issa Sewe alishinda kwa pointi dhidi ya Omari Bayi, katika pambano lao la raundi 4 uzani wa light weight,  Ambukile Chusa aliibuka mshindi dhidi ya  Emmanuel Kayala katika uzani wa super welter.

No comments:

Post a Comment