PARIS, Ufaransa
WIZARA ya Michezo ya Ufaransa imemsimamisha kazi Mkurugenzi wa Ufundi wa timu ya Taifa ya nchi hiyo kwa madai yake ya kwamba, shirikisho hilo limekuwa likiwajaza
wachezaji wenye asili ya Afrika na Waarabu katika timu ya Taifa.
Kwa mujibu wa taarifa ya pamoja ya Wizara na Shirikisho hilo (FFF), Francois Blaquart, ametimuliwa wadhifa huo ndani ya siku nane kutokana na kauli hiyo ambayo inaonekana ni ya ubaguzi wa rangi.
Hata hivyo, Blaquart alikiambia kituo cha redio cha RTL kuwa, kwa ujumla amefadhaishwa na kufukuzwa huko.
“Najisikia kuumia ,” alisema Blaquart . “Ila ninasubiri maamuzi ya tume ya uchunguzi," alisema kocha huyo, kabla ya kuongeza kuwa, mara zote yeye huwa siyo mbaguzi.
Hatua hiyo imekuja baada ya uchunguzi wa tovuti ya Mediapart kueleza kuwa, maofisa wa ngazi ya juu katika shirikisho hilo wamepitisha mapendekezo ya kupunguza asilimia 30 ya wachezaji wenye asili ya Afrika na Kaskazini mwa Afrika kuanzia umri wa miaka 13, katika michuano ya mbalimbali.
Mediapart inadai kuwa, Blaquart na kocha wa timu ya Taifa, Laurent Blanc, ndiyo waliopitisha maadhimio hayo ya kupunguza wachezaji kwenye vituo vya michezo na kwenye maeneo mbalimbali ya soka.
Blaquart aliiambia redio RTL: “Katika kikao kama hiki kama kuna vitu vinarekodiwa na kutolewa hadharani katika mazingira haya ya kashfa, kunazua maswali mengi kuhusu uadilifu wa wafanyakazi,”
Taarifa zinaeleza kuwa, uamuzi wa kumsimamisha kazi Blaquart umechuliwa kwa pamoja na Waziri wa Michezo, Chantal Jouanno na Rais wa FFF, Fernand Duchaussoy.
No comments:
Post a Comment