Na Suleiman Abeid, Shinyanga
BAADHI ya wakazi wanaoishi katika vijiji saba vilivyopo katika eneo linalodaiwa kuwa ni la hifadhi ya wanyama pori wilayani Meatu mkoani Shinyanga wamepinga amri ya serikali inayowataka kuhama kwa madai kuwa amri hiyo inapingana na haki za binadamu.
Kutokana na hali hiyo wakazi hao kutoka vijiji vya Mwabagimu, Makao, Mwangudo, Irambandogo, Sapa, Jinamo na Mbushi tayari wamefungua kesi katika Tume ya Haki za binadamu (LHRC) wakipinga amri hiyo iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Meatu, Bw. Abiudi Saideya.
Kwa mujibu wa nakala ya barua Kumb. Na. LHRC/LAC/11/589/01 ya Mei 12, mwaka huu iliyoandikwa na mwanasheria wa tume ya haki za binadamu kwenda kwa Bw. Saideya, wakazi hao wanaomba kusitishwa mara moja kwa amri hiyo mpaka pale watakapokuwa wametendewa haki.
Katika barua hiyo iliyosainiwa na Wakili Fulgence Massawe, wakazi hao wanadai amri iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya kuwataka kuhama kutoka katika makazi yao ndani ya siku 30 bila malipo yoyote ya fidia wala kupangiwa maeneo mbadala ya kwenda kuishi inapingana na haki za binadamu huku wawekezaji wakithaminiwa zaidi.
Wakazi hao wanadai wamekuwa wakiishi katika maeneo hayo kwa miaka mingi ambapo sehemu kubwa wamezaliwa hapo na hata makaburi ya babu na baba zao yapo katika maeneo hayo na kwamba amri ya kuwataka wahame ghafla bila ya kuwapatia maeneo mengine ya kuishi ni kuwafanya waishi maisha ya kutanganga katika nchi yao.
Aidha wakazi hao wanadai kitendo cha kuhamishwa kwao kinatokana na maeneo hayo kupewa mwekezaji ili aweze kuendesha shughuli za kitalii na kwamba utaratibu mzima wa kutolewa kwa maeneo yao kwa mwekezaji haukuwashirikisha kikamilifu wanavijiji kama sheria za uwekezaji zinavyoelekeza.
Kutokana na hali hiyo serikali imeombwa kusitisha kusudio lake na imetakiwa kabla ya kuwahamisha wanavijiji hao kwa nguvu basi kwanza zifanyike taratibu za kuwalipa fidia ya makazi na mali zao mbalimbali zisizohamishika zilizopo katika maeneo hayo na pia wapatiwe eneo mbadala la kwenda kuishi vinginevyo watakwenda mahakamani.
Kwa upande mwingine serikali imeombwa kufanya utafiti na tathimini katika eneo la vijiji hivyo, ili iweze kufahamika eneo halali ambalo linastahili kuwa chini ya maeneo ya Hifadhi ya Jamii (WMA) na ni eneo lipi mbadala ambalo wanavijiji hao watapaswa kuhamishiwa.
Hivi karibuni Bw. Saideya alitoa amri inayowataka wanavijiji hao kuhama mara moja katika makazi wanayoishi ndani ya siku 30 vinginevyo nguvu za ziada zitatumika katika kuwahamisha.
No comments:
Post a Comment