27 May 2011

Bin Hammam, Warner kuwekwa kiti moto FIFA

ZURICH, Uswizi

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Ulimwenguni (FIFA),  limeanza uchunguzi wa tuhuma za rushwa zinazozingira maofisa wake, akiwemo Makamu wa Rais wa
shirikisho hilo zilizotolewa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Chuck Blazer.

Katika shutuma hizo, Blazer alidai taratibu za maadili ya FIFA zilikiukwa katika mkutano unaoonekana uliandaliwa na Bin Hammam na Warner.

Maofisa wengine wawili ni Debbie Minguell na Jason Sylvester kutoka Muungano wa Soka wa nchi za Caribbean.

Mkutano uliofanyika Mei 10 na 11, mwaka huu  ulihusiana na uchaguzi wa Rais wa FIFA utakaofanyika Juni Mosi mwaka huu.

Bin Hammam, ambaye ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Asia, anawania nafasi ya urais wa FIFA dhidi ya rais wa sasa, Sepp Blatter, akitafuta nafasi ya kuwa kiongozi mpya wa shirikisho hilo la soka duniani.

Maofisa hao wanne wameitwa kufika mbele ya kamati ya maadili ya FIFA mjini Zurich Mei 29, mwaka huu,  na tayari FIFA ilitangaza Claudio Sulser, ambaye ni Mkuu wa Kamati ya Maadili ya kuwa, hataongoza  kikao hicho kwa vile ni raia wa Uswizi, sawa na Blatter ambaye ni mpinzani wa Bin Hammam na badala yake, kikao hicho kitakuwa chini ya Naibu Mwenyekiti Petrus Damaseb, raia  wa Namibia.

No comments:

Post a Comment