16 May 2011

CCM Kilindi yalishangaa Baraza la Madiwani

Na Yusuph Mussa, Kilindi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kilindi kimeshangazwa na uamuzi wa Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya hiyo kuwasimamisha kazi wakuu wawili wa
idara badala ya sita kama walivyokubaliana kwenye kikao cha madiwani wa chama hicho.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo, Bw. Clement Chamoto alisema wao kama chama walibariki maamuzi ya Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango iliyoketi Aprili 21, mwaka huu ili kuwasimamisha wakuu wa idara sita.

Wakuu wa idara hao wanadaiwa kuisababishia hasara halmashauri hadi ya sh. milioni 700 kutokana na jengo la halmashauri hiyo kushindwa kukamilika kwa muda uliopangwa, huku likiwa limeshagharimu sh. bilioni mbili badala ya sh. bilioni 1.5 zilizokusudiwa.

“Kwa kweli kama chama tumeshangazwa na uamuzi wa baraza la
madiwani kuwasimamisha wakuu wa idara wawili badala ya sita ambao
walipendekezwa na Kamati ya Fedha kutokana na hasara iliyoipata halmashauri, lakini si kwamba kuna madiwani wamehongwa fedha ili kubadilisha uamuzi huo bali nadhani ni uelewa mdogo.

“Lakini kama chama ni lazima tuitishe Kamati ya Siasa ya Wilaya kujadili hili lililotokea ili lisijirudie tena, na pia ni lazima tuwape mafunzo madiwani wetu ili kupata uelewa katika kuamua mambo mazito kama haya,” alisema Bw. Chamoto ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Kikunde.

Mbunge wa Kilindi, Bi. Beatrice Shellukindo alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema walijadili kwa kina kuhusu kusimamishwa kwa watumishi hao sita, wakaona kuna athari kubwa ndani yake hasa kama watumishi hao wataamua kuishtaki halmashauri katika kudai fidia ya kusimamishwa kazi na kudhalilishwa kwa kuhusishwa na ubadhirifu wa fedha.

“Tumeona tunaweza kujikuta halmashauri yetu inashtakiwa na kutakiwa kulipa fidia kwa watumishi sita waliosimamishwa, hivyo mimi kama
mbunge nilishauri mambo mengi kuona tunaondoka kwenye mtego ambao unaweza
kuifikisha halmashauri yetu mahali pabaya, hivyo tukaona hao wawili
waliosimamishwa walistahili, lakini sio kuongeza wengine,” alisema Bi.
Shelukindo.

Akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani kilichowasimamisha
watumishi wawili mei 3, mwaka huu, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Bw. Mussa Semdoe alisema hawakuwa na ugomvi na Kamati ya Fedha kutaka
kuwasimamisha wakuu wa idara sita, lakini wamezingatia maslahi ya halmashauri.

Wakuu wa Idara waliosimamishwa kutokana na sakata hilo ni
Afisa Maliasili na Mazingira ya Wilaya, Bw. Linus Mtefu ambapo imedaiwa wakati anakaimu nafasi ya Mkurugenzi wa Wilaya hiyo akidaiwa kuidhinisha malipo kinyume cha utaratibu na Mhandisi wa Wilaya, Bw. Simeoni Kasumo.

2 comments:

  1. Hawa Madiwani wa Kilindi hawana jambo lolote zaidi wanaingiza UKABILA kwenye kwenye Halmashauri hiyo wamewaondoa Kaimu Mkurugenzi na Mwekahazina na kumkaimisha kaimu mweka hazina wa kabila lao, na hii migogoro imenza tangu zamani kwani Mwenyekiti wa Halmashauri Bwana Mussa Semdoe amekuwa akimkandamiza sana Mweka hazina Bwana MUSSA NYEJI na amekuwa akimpangia majukumu, kama vile pale anapokuwa safari na kumwambia akiwa safari amkaimishe mtu anayemtaka yeye, Mimi kama Mwananchi wa Wilaya hii nimeona yote hayo na mara baada ya kumng'oa kwa mbinu ambazo wamezitaka wao wameamua kumkaimisha Bwana Grasford Kiweri kuwa mwekahazina ili wao waweze kumtumikisha wanavyotaka wao kwanza ni KABILA LAO, na zaidi ya hayo nimeshuhudia vikao visivyo rasmi wanavyo kaa "Mbunge Bitrice Shellukindo, Mwenyekiti wa Halmashauri Mussa Semdoe, kaimu Mwekahazina Bwana Grasford Kimweri na baadhi ya Madiwani wanaopanga kuwang'oa kabisa Bwana Linus Mtefu (Kaimu Mkurugenzi) na Mussa Nyeji (Mwekahazina, walivyo kuwa wanakaa katika baa moja ya ENKARE PUB iliyopo Wilayani humo. Na zaidi Mkoani wamepiga hesabu na kutamka wazi kwamba Hakuna ubadhilifu uliotokea lakini wao bado wanang'ang'ania msimamo wao huohuo je? Kunanini hapo?

    ReplyDelete
  2. Mbunge, Madiwani, Mwenyekiti wa Halmashauri wanalao jambo hakuna kingine tunaomba serikali iliangalie kwa umakini kwani hii Halmashauri inataka kuingiliwa na hao watu wanachotaka wao ni kujinufaisha wao.

    wakuu wa Idara ni wengi wanaotakiwa kuwajibishwa kama kunaubadhilifu kwanini wachaguliwe hao tu?

    Halmashauri si sehemu ya kuingiza siasa na UKABILA wanajiona wanajenga kumbe wanabomoa.

    SERIKALI ILISIMAMIE HILI KWA UMAKINI KWANI KUNA UKABILA NDANI YA HILI.

    ReplyDelete