17 May 2011

Mwaffisi 'ajivua gamba' BFT

Na Mwali Ibrahim

OFISA Habari wa Shirikisho la Ngumi za Ridhaa Tanzania (BFT), Eckland Mwaffisi amejiuzulu wadhifa huo kwa madai kukiukwa maamuzi ya vikao vya shirikisho
hilo.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwaffisi alisema ameamua kufikia uamuzi huo kutokana na kuona maamuzi mbalimbali ya Kamati ya Utendaji yakipelekwa kinyume na kamati hiyo yenye dhamana ya kuendeleza mchezo huo na si kiongozi mmoja au wawili katika BFT.

Alisema kutokana na ukweli huo, ndiyo maana kumekuwa na vikao halali ambavyo wajumbe hutumia muda mwingi kuzungumzia maendeleo ya mchezo huo na kutoa maamuzi mbalimbali.

Mwaffisi alisema, kutokana na ukiukwaji huo unaofanywa na kiongozi mmoja kwa maslahi yake binafsi ndiyo maana ameamua kuachia ngazi katika wadhifa huo.

"Sipo tayari kufanya kazi na viongozi wanaotumia nafasi zao kukwamisha juhudi za serikali na wadau wa michezo katika kuhakikisha heshima ya mchezo huu nchini unashuka na kujaribu kuurudisha kama ilivyokuwa zamani," alisema Mwaffisi.

Alisema, si busara kwa kiongozi kubatilisha maamuzi ya kikao halali, kati ya BFT na serikali kwa kivuli cha nafasi yake ili wajumbe na viongozi wengine waonekane wabaya kwa wachezaji, makocha na wadau wa michezo.

No comments:

Post a Comment