Na Elizabeth Mayemba
MABINGWA wapya wa Tanzania Bara, Yanga jana walipata mapokezi makubwa kutoka kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo waliofurika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Yanga ilikuwa jijini Mwanza kumalizia mechi yake ya mwisho ya Ligi Kuu Tanzania Bara, dhidi ya Toto African na kushinda mabao 3-0, ambayo yaliiwezesha kuizidi Simba bao moja na hivyo kutawazwa kuwa mabingwa wapya.
Wachezaji wa timu hiyo waliwasili jijini Dar es Salaam jana saa 8 mchana, ambapo walilakiwa na wanachama pamoja na mashabiki wao huku wakiwa na kombe lao, ambapo moja kwa moja waliongoza mpaka Makao Makuu ya klabu hiyo mitaa ya Twiga na Jangwani.
Msafara wa wachezaji hao ulikuwa na magari yasiyopungua 20, pikipiki aina ya Bajaji na pikipiki za kawaida huku mashabiki wakiwa wamevalia fulana zilizoandikwa Yanga bingwa.
Mashabiki hao walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za kuisifu timu yao pamoja na kuwatania mahasimu wao Simba, ambapo waliwataka wakaukatie rufani ubingwa wao.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuwasili uwanjani hapo, Kocha Mkuu wa timu hiyo Mganda Sam Timbe alisema kazi ya kutwaa ubingwa ilikuwa ngumu kwao, lakini bidii ya wachezaji wake mazoezini ndiyo iliyowafikisha hapo walipofikia.
Alisema awali walishaukatia tamaa ubingwa na kuwaachia Simba ambao walikuwa wamewazidi kwa pointi nne, lakini walipopoteza mechi zao mbili, ambazo walilazimishwa sare waliongeza bidii na hatimaye wametwaa ubingwa.
"Kwanza kabisa ninawashukuru wachezaji wangu, ambao walifuata maelekezo yangu na hatimaye tumechukua ubingwa, pia nawashukuru wana-Yanga wote ambao tulishirikiana kipindi chote ambacho tulikuwa tunacheza na haya ndiyo matunda yake," alisema Timbe.
Naye nahodha wa timu ya Yanga, Shadrack Nsajigwa alisema wamefurahi kutwaa ubingwa, kwani walishakata tamaa lakini kocha wao aliwapa moyo na kuwataka wajitume zaidi kwa kuwa ubingwa hauna mwenyewe.
"Kocha alifanya kazi ya ziada sana kwetu, kwani tulijua ubingwa ni wa Simba, lakini kocha alitutia moyo matokeo yake tumeyaona tumejenga heshima kubwa kwa mashabiki wetu," alisema Nsajigwa.
No comments:
Post a Comment