12 April 2011

Mbunge: Vigogo wananufaika na mgawo wa umeme

Na Reuben Kagaruki

MAKAMU Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu ya Mashirika ya Umma, Bw. Deo Filikunjombe amefichua siri kuwa kuna watu wananufaika na mgawo wa
umeme unaendelea nchini wakiwemo viongozi wa serikali.

"Nina ushahidi wapo viongozi wa serikali wanakwamisha mradi wa makaa ya mawe yaliyopo Ludewa kwa kuwa wananufaika na mgawo wa umeme unaotokea mara kwa mara nchini," alisema, Bw. Filikunjombe.

Akizungumza kwenye mkutano wa wakazi wa Ludewa waishio Dar es Salaam jana, mbunge huyo alisema kuna makundi ya kisiasa  yanayokwamisha uzalishaji wa umeme na miongoni mwao wapo wanaotaka urais mwaka 2015.

"Wanafanya hivyo ili ionekane serikali haifanikiwi... tumewaita kwenye kamati na kuwaambia waache," alisema na kuongeza;

"Tumefanya utafiti wa kutosha na kufanikiwa kupata nyaraka na barua ambazo zinakwamisha mradi ya Liganga na Mchuchuma.

Alisema sera ya TANESCO ni kuanza kuzalisha umeme wa makaa ya mawe ifikapo mwaka 2025, jambo ambalo haliwezi kukubalika kwa kipindi chote hicho nchi iwe inaendelea kukumbwa na mgawo wa umeme.

"Pamoja na vuta nikuvute za hapa na pale, leo ninayo furaha kuwaambieni kwamba kupitia waraka wa Baraza la Mawaziri wa kikao kilichopita, serikali imekubali rasimi kuiendeleza miradi ya Liganga na Mchuchuma kwa kushirikiana na mwekezaji mkubwa kutoka China-Sichuan Hongda," alisema Bw. Filikungombe.

Alisema lengo lao kwa sasa ni kuhakikisha mkataba unasainiwa mwezi huu ili mwekezaji awe Ludewa mapema mwezi wa saba, mwaka huu.

"Lengo ni kuona ifikapo mwaka 2013 umeme unazalishwa kutoka Mchuchuma na ifikapo mwaka 2014 Chuma kinachinbwa Mundindi ifikapo mwaka 2015," alisema.

1 comment:

  1. Tunashukuru kuliona hilo kwani lilikuwepo siku nyingi na hujuma zipo tokea 2005,kwani
    hakuna umadhubuti wa kufatilia kwa kina watu wapo maofisini wanawatuma watu kwenda Mtera,kihansi na hale nk, wewe umekaa unangoja ripoti hushangai kuona hata kamati inapofatilia kujuwa tatizo ninini waziri haachi kuwa nao bega kwa bega? nia siri isivuje!!Mitambo huzimwa kuambiwa mara mibovu au maji yamepunguwa hivi hushangai mvua zote hizi maji hayaja ongezeka maji yote yanaelekea wapi?na kama yamepoteza mwelekeo ni nani aliyeyapoteza kama si hujuma?!!

    ReplyDelete