11 April 2011

Yanga mabingwa Tanzania Bara

*'Simba mwaka wa shetani'

Na Marry Ng'oboko, Mwanza

YANGA jana imetangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya kuifunga Toto African mabao 3-0 katika mechi ya
ligi hiyo iliyochezwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa.

Mabingwa hao wapya wamenyakua ubingwa huo kutokana na kuongoza ligi hiyo kwa tofauti ya bao moja dhidi ya watani wao wa jadi Simba, ambao nao walishindwa kutangazwa kuwa mabingwa baada ya kuifunga Majimaji ya Songea mabao 4-1, mabao ambayo ni pungufu kwa Yanga.

Katika ligi hiyo Yanga imefungwa mabao saba na kufunga 32, ambayo ni wastani mzuri katika mabao ya kufungwa tofauti na Simba ambayo imefungwa mabao 16 na kufunga40.

Mechi ya jana timu zote ziliingia uwanjani na kucheza taratibu katika kipindi cha kwanza, ambapo wachezaji wote walionekana kucheza kwa hadhari kubwa.

Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga, kuingia kwa nguvu na kufanikiwa kupata bao la kwanza dakika ya 46, lililopachikwa kimiani na Nurdin Bakari, baada ya kupiga adhabu ambayo mpira ulikwenda moja kwa moja wavuni.

Baada ya bao hilo, Yanga iliendelea kuliandama lango Toto na kufanikiwa kupata bao la tatu dakika ya 63, lililofungwa na Mzambia Davies Mwape kwa shuti kali.

Kuingia kwa bao hilo, kuliwaamsha wachezaji wa Toto ambao walikuja juu kutaka kusawazisha mabao hayo, lakini hata hivyo ukuta wa Yanga ulikaa imara kuondoa hatari zote zilizopelekwa langoni mwao.

Yanga iliandika bao la tatu lililoipa ubingwa timu hiyo, dakika ya 89 kupitia kwa Nurdin ambaye alikutana na mpira uliopigwa na Shedrack Nsajigwa baada ya kutokea piga nikupige katika lango la Toto African.

Baada ya kunyakua ubingwa huo, Yanga ilikabidhiwa Kombe na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abbas Kandoro ambaye aliwatakia mafanikio mema huko waendako katika michuano ya kimataifa.

Naye Zahoro Mlanzi anaripoti kutoka Dar es Salaam kuwa, timu ya Simba imeshindwa kutetea ubingwa wake baada ya kuifunga Majimaji ya Songea kwa mabao 4-1.

Katika mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kubisha hodi langoni mwa Majimaji kwa kufunga bao dakika ya 11 lililofungwa na Shija Mkina, akimalizia krosi ya Emmanuel Okwi.

Simba ambayo ilionekana kuhitaji ushindi kwa udi na uvumba, ilifunga bao la pili dakika ya 24 kupitia kwa Okwi, akimalizia pasi ya Ali Ahmed 'Shiboli'.

Majimaji ilitulia na kufanya shambulizi la nguvu dakika ya 34 kupitia kwa Kassim Kilungo, ambaye aliunganisha vibaya kwa kichwa kona iliyopigwa na Ulimboka Mwakingwe.

Dakika nne kabla ya mapumziko, Simba ilipata pigo baada ya beki Meshack Abel, kutolewa nje kwa kadi nyekundu na Mwamuzi Alex Mahagi kutoka Mwanza kwa kumchezaea vibaya Mohamed Kijuso, ndani ya eneo la hatari na Kilungo kukwamisha mpira wavuni kwa mkwaju wa penalti.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku kila timu ikifanya mashambulizi lakini dakika ya 55, Paul Ngalawa alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kumkwatua Mkina.

Simba ilifunga bao la tatu dakika ya 74 kupitia kwa Mbwana Samatta, aliyeingia badala ya Mkina akimalizia kazi nzuri iliyofanywa na Okwi na dakika 10 baadaye Kulwa Mobi wa Majimaji naye alitolewa nje kwa kadi nyekundu.

Bao la nne la Simba lilifungwa na Okwi, katika dakika tano za ziada akipokea pasi safi ya Jerry Santo lakini licha ya kuibuka na ushindi huo mnono, imeshindwa kutetea ubingwa kwa tofauti ya mabao ya kufungwa na kufunga.

Simba itajutia nafasi iliyoipata katika dakika za lala salama baada ya Santo, kuangushwa ndani ya eneo la hatari na mwamuzi Mahagi kuamuru ipigwe penalti lakini Okwi alishindwa kukwamisha mpira wavuni.

Kutoka Uwanja wa Manungu Mkoani Morogoro, Thobias Kifaru ambaye ni Ofisa Habari wa Mtibwa Sugar anaripoti kuwa Mtibwa Sugar imeibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya African Lyon.

Mabao yote ya Mtibwa yalifungwa na Thomas Morris, katika dakika za 14 na 74.

Kutoka Uwanja wa Jamhuri Mkoani Morogoro, Omari Mngindo anaripoti kuwa, timu ya Azam FC imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting. Mabao ya Azam yalifungwa na John Bocco 'Adebayor' dakika ya 46 akiunganisha krosi ya Mrisho Ngassa.

Ruvu ilisawazisha dakika ya 48 kupitia kwa Mfaume Jumanne akiunganisha krosi ya Said Madega na la ushindi la Azam lilifungwa dakika ya 71 na Ngassa.

Kutoka Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Benedict Kaguo anaripoti kuwa JKT Ruvu imetoka sare na Polisi Dodoma kwa kufungana bao 1-1.Bao la JKT lilifungwa na Mwinyi Kazimoto dakika ya 13 na lile la kusawazisha la Polisi lilifungwa dakika ya 55 kupitia kwa Bantu Nsungwe.

Kutoka Uwanja wa Kaitaba, Bukoba wenyeji Kagera Sugar walilazimishwa suluhu na Arusha FC.

4 comments:

  1. Dewji anaiburuza team ya Simba. Mpatie nafasi yake Phiri na kazi itaonekana. Tusitumie uwezo wetu kifedha kutwala. kinachohitajika ni ujuzi na busara, baadaye hela na kujituma. Simba kuna maneno mengi kuliko matendo. Pamoja na hayo, Wachezaji wa simba waeathirika kisaikolojia na wanahitaji ushauri wa kisaikolojia. I think Phiri will look into that.

    ReplyDelete
  2. Hivi hawa tff walijuaje kama yanga itachukua ubingwa na kuandaa kombe uwanjani!mi sipati jibu hapo ila naona giza tuuuuuuuuuuuu

    ReplyDelete
  3. makombe yalikuwa mawili yameandaliwa moja mechi ya simba na majimaji na lingine mechi ya yanga na toto... so walifanya kitu kilichokwenda shule.... umeshaela sasa!1
    YANGA OYEE! CCM OYEE! DAR OYEE!!! JANGWANI OYEEE!! ILALA OYEEE!!TANZANIA OYEEE.... BENDERA YA CCM OYEEE!! SAM TIMBE OYEEE! jamani yanaga mmenipa raha ya kuongea leo

    ReplyDelete
  4. CCM oyee nini? wana nini cha ziada kama si tu wizi wao! nawe pia jizi nini?

    ReplyDelete