Na Elizabeth Mayemba
KOCHA Msaidizi wa timu ya ya taifa ya Uganda 'The Cranes', Moses Basena, ameteuliwa na Kamati ya Utendaji ya Simba, kuchukua mikoba ya Kocha
Mzambia Patrick Phiri.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa klabu ya Simba, Ismail Rage, alisema Basena ataanza rasmi kibarua chake Mei 5, mwaka huu, na ataingia mkataba wa majaribio wa miezi sita.
"Kamati ya Utendaji ya Simba imemteua Bassena kutoka Uganda kuwa Kocha Mkuu wa timu yetu, ataingia mkataba wa majaribio ya miezi sita kuanzia Mei Mosi mwaka huu," alisema Rage.
Alisema baada ya kocha huyo kutua nchini, ndiye atakuwa na jukumu la kumtafuta kocha msaidizi atakayesaidiana naye na ataupa uongozi taarifa za msaidizi wake aliyempata.
Rage alisema hatua ya kutafuta kocha mpya imekuja baada ya Phiri kumaliza mkataba wake na alipoongezewa mkataba mpya, hakuusaini wala kuurudisha kwa uongozi, hali ambayo inaonesha kwamba, hapendi kuendelea kuinoa timu yao.
Alisema pamoja na kutafuta kocha mpya, pia wamefumua benchi nzima la ufundi, hivyo kuanzia sasa hakuna tena benchi la ufundi mpaka kocha wao mpya atakapoanza kazi rasmi.
Mwenyekiti huyo alisema, baada ya kupitia kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), wamegundua kwamba, hakuna nafasi ya Meneja wa timu, zaidi ya kocha.
Pia, alisema mchakato wa kuanza kwa usajili wa wachezaji wao wapya unaendelea, na kwamba hadi sasa hakuna mchezaji wao hata mmoja waliyemuacha na wote wana mikataba, isipokuwa Rashid Gumbo ambaye mkataba wake umemalizika.
Rage alisema Kamati ya Utendaji imewaandikia barua ya onyo wachezaji wake, Mussa Hassan 'Mgosi' na Kelvin Yondani, kwa utovu na nidhamu, na pia watakuwa wakilipwa nusu mshahara.
Alisema Mgosi ana tabia ya kuzungumza ovyo na vyombo vya habari, na Yondani alitoroka kambini siku moja baada ya mchezo wao na TP Mazembe na hajulikani alipo hadi sasa, na mara ya mwisho alipigana kambini kwa kugombea juisi.
No comments:
Post a Comment