12 April 2011

Watano wafa wakiiba petroli Singida

*Ni baada ya gari la mafuta kupata ajali

Na Jumbe Ismailly, Manyoni

WATU watano wamekufa papo hapo na wengine 46 kujeruhiwa vibaya huku wengine wakibakia majivu na mafuvu baada ya kuungua moto petroli uliolipuka wakati
wakijaribu kuiba mafuta kwenye gari aina ya fuso lililogonga injini ya treni.

Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Bw. Ally Rufunga alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 11 jioni kwenye makutano ya reli na barabara iendayo Singida na Itigi.

Alisema gari hilo lilibeba lita 40,000 za mafuta aina ya petroli kutoka Dar-es-Salaam kwenda Shinyanga lilipofika kwenye makutano hayo ya barabara liligonga injini ya kichwa cha treni kilichotoka kusindikiza treni ya mizigo kituo cha Aghondi.

Alisema dereva wa gari hilo hakuiona injini hiyo na hivyo kujikuta akiigonga na kusababisha matenki ya mafuta kutoboka na kuanza kutiririsha mafuta.

Baada ya ajali hiyo, wananchi wa mjini Manyoni walifurika kwenye eneo la tukio wakiwa wamebeba vyombo vya aina mbalimbali, zikiwamo ndoo na madumu kwa ajili ya kuiba mafuta hayo.

Alisema licha ya askari 10 waliokuwepo kwenye eneo hilo kuweka ulinzi, lakini ilipofika saa mbili usiku, askari walizidiwa nguvu na wananchi walioanza kuchukua mafuta, na ndipo ghafla tenki hilo lililipuka na kuanza kuwaka moto.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Singida, Bi. Celina Kaluba alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutaja namba za injini ya gari moshi kuwa ni T483 BLM na tela aina aina ya Iveco lenye namba za usajili T 312 BBH.

Alifafanua kuwa watu 10 walioko mahututi wamehamishiwa katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma, wengine 10 walipelekwa Hospitali ya Mkoa wa Singida, 10 Hospitali ya Mtakatifu Gasper ya Mji mdogo wa Itigi na 16 waliobakia wamebakia kwenye Hospitali ya Wilaya ya Manyoni.

"Kwa kweli ilikuwa vigumu kuokoa maisha ya watu waliokufa kwa sababu moto ulikuwa ukiwaka kwa nguvu na ilipofika saa sita usiku tulifanikiwa kuokoa miili miwili ambayo ilitambuliwa na kupelekwa hospitalini. Maiti mbili zilibaki kichwa na hazikutambuliwa," alisema Bi. Kaluba.

Alisema kuwa wananchi walikuwa wanakatazwa na askari kusogea karibu na eneo la tukio lakini waliwazidi nguvu na kuanza kuchota mafuta huku wengine wakiendelea kufuata vyombo vya kubebea mafuta hayo.

Aliwataja majeruhi 46, wakiwamo 13 ambao ni askari wa jeshi hilo, kuwa ni Selemani Shabani (34) mkazi Mwembeni, Issah Kiwande (29) mkazi wa mjini Manyoni, Jacob Juma (26), askari PC Mosses Philemon (26), Marius Kalumuna (23), Faustine Matimbwa(27) na Leornad Kajeni ( 19).

Wengine Juma Petro (23), Philipo Mwita (28), Zakaria Wilsoni (12), Hussein Ramadhani (14), Mikidadi Hemedi (26), Aron Andrew (15), Yoramu Wilson (33), Rashidi Hamisi (40) PC Alfani John (28), Nehemia Jonasi (20), Akley Jonas (25) na Kayanda Iddi (37).

Wengine ni PC Gifti (22), Mhembeno Mahanya (26), Afande Stanley (22), Mohamedi Hamisi (15), Hussein Hamisi (27), Afande John (27), PC George (22), Ally Hatibu (20), Huseini Sipi (22), Francis Labeni (16), Omari Abdala (18) Adinani Athumani (23), Ayoubu Yahaya (24), Hamidi Yahaya (26), Farahani Juma (23), Mwami Paulo (22) na Juma Waziri (28).

Wengine ni PC Xavery Emanueli(24),Mwidini Huseni(38),Anuse Kabyuke (35), PC Alfayo John (28), Aroun Ado (15), Kitwana Juma (22),Mashaka Ulange (15), Rashidi Abedi (20) na Amasi Abubakari.

Kwa upande wake, shuhuda Kasongo Logina mkazi wa Mtaa wa Samaria, alisema licha ya ulinzi uliowekwa na askari hao, kilichowakera wananchi ni vitendo vya askari hao kuanza kuwauzia mafuta hayo kwa sh. 10,000 kwa dumu moja la lita 20, na kusababisha watu kulundikana kwenye eneo hilo kununua mafuta.

"Unajua kuwa usalama ulikuwepo, cha kushangaza ilipofika mida ya saa tatu usiku askari hao walianza kutuuzia mafuta na kusababisha mlundikano wa watu ili waweze kununua mafuta hayo kwa bei rahisi na wao waende kuuza kwa bei ya juu zaidi," alisema Kasongo.

Baadhi ya polisi waliohojiwa na gazeti hili walidai kuwa mshahara mdogo kwa hiyo waliamua kufanya biashara ya mafuta ili waweze kufidia mshahara wao.

“Mzee kama unavyojua kwamba tunalipwa mishahara midogo sana kwa hali hiyo tuachie tutafute riziki ya kujiongezea maslahi yetu kwa kuuza mafuta haya ili tuweze kujilipa mishahara mizuri angalau kwa leo" alisisitiza mmoja wa askari hao.

5 comments:

  1. Aroo "Geshi" rimeaibika kweri.

    ReplyDelete
  2. Aha! Kumbe hii ndo dhana ya uulinzi shirikishi! Askari wanashiriki katika uhalifu na maatookeo yake ndiyo hayo! Afande Mwema nadhani ni bora ukaja na dhana ingine ya ulinzi shirikishi! Sijawahi kuona mahali pengine popote ambapo polisi wamekosa maadili kama hapa kwetu TZ. Kamanda wa vituo husika wakiwajibishwa labda nao watawajibisha maofisa wao! Aibu sana kwa jeshi linalotakiwa kuwalinda wananchi linapowaingiza kwenye ualifu!

    ReplyDelete
  3. Ukiwawajibisha askari polisi baasi utawajibisha jeshi lote maana hivyo ndivyo walivyo!

    ReplyDelete
  4. Sie nasi mishahra yetu haitutoshi bsi tujiingize kwenye uhalifu?

    ReplyDelete