12 April 2011

Shahidi ambebesha Msabaha zigo la Richmond

Na Rabia Bakari

MTAALAMU wa Manunuzi na Katibu wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme nchini (TANESCO), Bw. Nicolau Shuke (55) amedai kuwa Kampuni ya Richmond ilipewa
zabuni kuzalisha umeme nchini kwa maelekezo kutoka kwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Ibrahimu Msabaha.

Bw. Shuke ambaye ni shahidi wa kwanza katika kesi hiyo, alidai hayo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana alipokuwa akitoa ushahidi katika kesi ya kughushi na kutoa taarifa za uongo kuhusu Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura ya Richmond inayomkabili Mfanyabiashara, Bw. Naeem Gire.

Alidai kuwa alidai kuwa kwa wadhifa huo katika bodi alikuwa na majukumu ya kuratibu shughuli zote za bodi, kuitisha vikao, na kutekeleza maamuzi yanayofikiwa na bodi na mnamo mwaka 2006  alishiriki katika kukodisha mashine ya kufua umeme wa dharura ya megawati 100 kutokana na ukame wa muda
mrefu nchini, uliosababisha upungufu wa umeme hivyo serikali kupitia Tanesco kukodisha mitambo hiyo.

Shahidi huyo alidai kuwa idara inayoshughulikia miradi ya TANESCO ilitengeneza nyaraka za kuanzisha mchakato wa kutangaza zabuni ya manunuzi ambayo ilitangazwa kwenye gazeti kama zabuni ya ushindani ya kimataifa.

“Kampuni ya Richmond ilifuata utaratibu huo ambapo ilikuwa moja kati ya kampuni nane zilizopokelewa na kufanyiwa uchambuzi na kamati maalumu ambapo iliwasilisha mkataba kati yake na kampuni ya Pratt&Whitney Power System, mchoro wa kiufundi, vipeperushi vinavyohusiana na mashine hiyo, barua
yenyewe ya tenda, na ile inayompa mamlaka kisheria Naeem Gire kusimamia,” alidai.

Aliieleza Mahakama kuwa mchakato wa kuchanganua zabuni hiyo uliundwa kwa mujibu wa sheria chini ya Mwenyekiti Boniface Njombe na wawakilishi wawili aliowataja kwa majina Poule na Humke kutoka kampuni ya Lahmaye ya Ujerumani.

Alidai kuwa baada ya uchambuzi matokeo yaliweka wazi kuwa hakuna mshindi aliyefikia vigezo vilivyowekwa ambapo bodi iliridhia uongozi wa Tanesco ujulishwe kuwa hakupatikana mshindi wa zabuni hiyo.

“Baada ya serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini  kujulishwa kuwa hakupatikana mshindi walielekeza wapelekewe nyaraka za zabuni ambapo ilitengeneza mchakato wake maalumu kusimamia zabuni hiyo.

“Lakini kabla mchakato huo haujaanza yakaibuka malumbano kati ya serikali na Tanesco kwamba zabuni itangazwe kwa siku 10 au zaidi. Tulivyoona sheria inavunjwa tuliwajulisha PPRA ambao walishauri kuwa haiwezekani kutangaza zabuni ya kimataifa kwa siku chache hivyo, lakini serikali ilisisitiza kuwa agizo la siku 10 litekelezwe,” alidai shahidi huyo.

Aliongeza kudai kuwa kwa mujibu wa sheria ya manunuzi ya mwaka 2004 inaelekeza kuwa zabuni inapaswa itangazwe kwa siku 45 lakini hii ilitangazwa kwa siku 10 kwa maelekezo ya Waziri Msabaha.

Kesi hiyo iliyoanza kusikilizwa kwa mara ya kwanza jana mbele ya Hakimu Waliarwande Lema itaendelea tena leo.

Katika kesi hiyo, Gire anadaiwa kutoa taarifa za uongo kuwa kampuni hiyo ya Richmond ina uwezo wa kuzalisha megawati 100 za umeme wakati akijua kuwa si kweli.

Msitakiwa pia anadaiwa kughushi na kumruhusu Mwenyekiti wa Development Company LLC ya Texas Marekani, Mohamed Gire, afanye shughuli za kampuni hiyo hapa nchini.

Mbali na hilo, mshitakiwa anadaiwa kuwadanganya wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kwamba Kampuni ya Richmond ina uwezo wa kuzalisha megawati 100 za umeme nchini Tanzania ili kampuni hiyo iweze
kupendekezwa na wajumbe hao.

No comments:

Post a Comment