Na Mohamed Hamad, Manyara
JESHI la Polisi wilayani kiteto mkoani Manyara linawashikilia wakazi wawili wa kijiji cha Lortepes wilayani hapo kwa tuhuma za kumnyonga mwanafunzi wa darasa la kwanza
wa Shule ya Msingi Lotapesi wakitaka kuiba mifugo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Kamanda wa Polisi mkoani Manyara, Bw. Parmena Sumary alisema watu hao walikamatwa juzi katika kata ya Sunya wilayani humo.
Kamanda Sumary alisema watu hao wanadaiwa kufanya matukio hayo Aprili 16, mwaka huu kwenye mbuga ya Mbayeki Kata ya Sunya na kuiba ng'ombe 700 na mbuzi 200.
Alisema watu hao walidaiwa kumuua kwa kumnyonga mtoto huyo, Noel Simon (13) kwa kutumia shuka aliyokuwa amevaa na kumjeruhi mdogo wake Naishoo Simon (10) shingoni kwa panga.
Alisema wezi hao ambao hakutaja majina yao wa madai madai kuwa yataharibu uchunguzi wanaendelea kuhojiwa.
“Watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na bado tunaendelea na uchunguzi wa tukio hili kabla ya kuwafikisha mahakamani ili wajibu mashtaka ya mauaji na wizi wa mifugo,” alisema Kamanda Sumary.
No comments:
Post a Comment