13 April 2011

Azzan kuwaongoza Kaseba, Maugo Jumamosi

Na Addolph Bruno

MBUNGE wa Jimbo la Kinondoni ambaye pia ni mdau wa michezo, Idd Azzan anatarajia kuwa mgeni rasmi katika pambano la ngumi litakalowakutanisha mabondia
Japhet Kaseba na Mada Maugo, litakalofanyika Jumamosi katika Ukumbi wa PTA Sabasaba Jijini Dar es Salaam.

Pambano hilo lisilo la ubingwa linatarajia kuwa ni la uzani wa kati (middle) kg. 72 ambapo mshindi ataandaliwa kucheza na Francis Cheka, ambaye kwa sasa yupo katika maandalizi ya kucheza na Mmarekani John Upshaw hivi karibuni.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mratibu wa pambano hilo, Siraji Kaike alisema maandalizi yanaendelea vizuri ikiwa ni pamoja na mabondia wote wapo katika hali nzuri na wanaendelea na mazoezi.

Alisema awali Kamanda wa Kanda Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye pia ni mlezi wa mchezo huo hapa nchini, Suleiman Kova alitarajiwa kuwa mgeni rasmi katika pambano hilo, lakini kutokana na kuzidiwa na kazi, nafasi yake itachukuliwa na Azzan ambaye amethibitisha kushiriki.

"Tumefanya mazungumzo na mgeni rasmi yupo tayari kabisa kuja kusapoti na kila kitu kinakwenda vyema, wapenzi na wadau wote wakae sawa kutokana na kwamba tumeyamaliza matatizo yote na matarajio ni kwamba huu ni miongoni mwa michezo mizuri, iliyowahi kufanyika," alisema mratibu huyo huyo.

Alisisitiza kuhusu Maugo, kugoma kutokana na kuzidiwa kg. mbili na mpinzani wake madai hayo hayapo tena kwa kuwa Kamati ya Maandalizi ilikaa nao na kukubaliana Kaseba, afanye jitihada za kupunguza uzito jambo ambalo analitekeleza.

No comments:

Post a Comment