*Utafiti wabaini wako hatarini kupoteza nafasi zao
Na Tumaini Makene
UTAFITI uliofanywa juu ya utendaji kazi wa wabunge, katika bunge la tisa, umetoa tahadhari kwa wabunge wa bunge la 10 wasiochangia kukaa
mkao wa kutorudi bungeni, huku vyama vyao vikihadharishwa kuwa vitaadhibiwa kwa kuzidi kupoteza wawakilishi.
Tahadhari hiyo imetokana na utafiti huo kubaini kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, moja ya vigezo ambavyo wapiga kura walivitumia ilikuwa ni kuzingatia kiwango cha ushiriki wa wabunge katika bunge la tisa.
Kutokana na kuzingatia kiwango hicho cha kushiriki katika kuchangia mijadala, chama kilichokuwa na ushiriki mdogo bungeni, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeonekana kuadhibiwa kwa kupoteza viti vingi, ambapo chama kilichokuwa na ushiriki mkubwa bungeni (CHADEMA) kimefanikiwa kuongeza viti.
"Kidokezo kinachojitokeza katika matokeo haya kwa bunge la 10 ni kwamba vyama vya siasa vyenye nia ya kukua katika siku zijazo vitahitaji kuwahimiza wabunge wao kuwa washiriki wazuri katika shughuli za bunge," imesema sehemu ya utafiti huo uliofanywa na asasi binafsi maarufu ya Uwazi, iliyoko chini ya Twaweza.
Asasi hiyo ambayo imeshafanya tafiti mbalimbali, zilizoibua mijadala mikubwa nchini, ikiwa ni changamoto kwa wahusika, kama ule wa wahitimu wa darasa la saba kutoweza kumudu masomo ya darasa la pili, imetumia tovuti ya bunge katika kukusanya takwimu za taarifa yake hiyo.
Katika taarifa yake hiyo, ambayo Majira linayo nakala yake, Twaweza imesema kuwa zaidi ya nusu ya wabunge wa kuchaguliwa waliokuwepo katika bunge la 9 hawakurudi bungeni baada ya uchaguzi wa Oktoba 2010;
Huku pia wabunge ambao hawakuwa mawaziri au watumishi wenye nyadhifa za juu serikalini walikuwa na uwezekano mkubwa zaidi wa kutorudi bungeni, ambapo ni asilimia 35 pekee ya wabunge wa kawaida wamerudi katika bunge la 10.
Katika ripoti hiyo iliyopewa jina la 'Nani amerudi? Utendaji katika bunge na uwezekano wa wabunge kuchaguliwa kwa mara nyingine,' imesema kuwa chini ya nusu ya wabunge wa kuchaguliwa wamerudi tena bungeni mwaka 2010, huku wengi wao wakiwa ni waliokuwa na ushiriki mkubwa zaidi kuliko wale ambao hawakurudi.
"Muhtasari huu unaonesha kwamba nusu ya wabunge wa kuchaguliwa wamerudi tena bungeni katika mwaka 2010 na kwamba ni theluthi moja tu ya wabunge wa kuchaguliwa ambao si watumishi wenye nyadhifa za juu katika serikali waliofanikiwa kubaki na viti vyao.
"Unaonesha kwamba wabunge wa kuchaguliwa wa kawaida waliorudi bungeni ni wale waliokuwa na ushiriki mkubwa zaidi... Vile vile, muhtasari unaonesha kwamba vyama vya siasa vyenye wabunge wenye ushiriki mkubwa katika bunge vilipata viti vingi zaidi...;
"Katika uchaguzi wa Oktoba 2010 wakati chama chenye wabunge ambao hawakuwa na ushiriki mkubwa bungeni kilipoteza viti. Kwa pamoja, mambo haya yanaashiria kuwa utendaji wa wabunge ndani ya bunge una umuhimu mkubwa kwa wapiga kura," imesema sehemu ya taarifa ya utafiti huo.
Bunge la tisa, lilikuwa na wabunge wa kuchaguliwa wapatao 231, ambapo kati yao 100 ndiyo wamerudi, huku 131 (sawa na asilimia 57) hawakurudi.
Katika bunge hilo CCM kilikuwa na wabunge 186, CUF kilikuwa na wabunge 33, CHADEMA wabunge 11 na UDP mbunge mmoja. Wakati katika bunge la sasa, CCM kina wabunge 259, CHADEMA (48), CUF (36), NCCR-Mageuzi (4), UDP (1) na TLP (1).
Pia wabunge ambao ni mawaziri na watumishi wengine wenye nyadhifa za juu serikalini (kama vile spika, naibu spika, mwanasheria mkuu wa serikali na wakuu wa mikoa) walikuwa na nafasi nzuri zaidi ya kurudi bungeni kuliko wabunge wa kawaida.
"Asilimia 80 (ambao ni 35 kati ya 44) ya wabunge wa kuchaguliwa waliokuwa watumishi wenye nyadhifa za juu serikalini walichaguliwa, ambapo asilimia 35 tu (sawa na wabunge 65 kati ya 187) ya wabunge wa kawaida walirudi bungeni baada ya uchaguzi wa 2010," imesema ripoti hiyo.
Vyama vya CUF na CCM vilikuwa na asilimia kubwa zaidi ya wabunge ambao hawakurudi, ambapo asilimia 66 ya wabunge wa kawaida wa CCM hawakurudi bungeni baada ya uchaguzi, huku wabunge wa namna hiyo asilimia 67 kwa upande wa CUF nao pia hawakurudi, huku UDP na CHADEMA vikiwa na idadi ya chini zaidi katika kundi hili.
"Chama cha UDP ambacho mbunge wake pekee alirudi bungeni na CHADEMA (asilimia 40) ndivyo vilivyokuwa na asilimia za chini zaidi za wabunge wa kuchaguliwa wa kawaida ambao hawakurudi bungeni baada ya uchaguzi 2010."
Kwa mujibu wa utafiti wabunge wengi ambao hawakurudi bungeni baada ya uchaguzi mkuu walikuwa na ushiriki mdogo, ikioneshwa kuwa waliorudi walitoa wastani wa michango 92 ndani ya miaka mitano, wakati 'waliobwagwa' walichangia wastani wa michango 81.
"Kati ya wabunge wa kuchaguliwa wa kawaida 187 katika bunge la tisa, 65 wamerudi wakati 122 hawakurudi. Wastani wa michango iliyotolewa na wabunge waliorudi ilikuwa juu kidogo kuliko ile iliyotolewa na wabunge ambao hawakurudi.
Utafiti huo umekielezea CUF kuwa ndiyo chama pekee kilichorudisha bungeni wabunge wake wengi wenye ushiriki mkubwa, ambapo kwa tathmini ya ushiriki kichama iliyofanywa na Uwazi inaonesha kuwa chama hicho kimefanikiwa kurudisha wabunge wake wengi waliochangia sana.
"Iwapo mtu atathmini kiwango cha ushiriki wa wabunge waliorudi na wale ambao hawakurudi ki-chama, ataona kwamba ni CUF pekee ndiyo iliyorudisha bungeni wabunge wake wengi waliokuwa na ushiriki mkubwa. Wabunge 6 wa CUF waliorudi walichangia hoja kwa wastani wa mara 116...;
"Ambapo wabunge 12 ambao hawakurudi walichangia hoja wastani wa mara 72...CCM na CHADEMA hakuna tofauti kubwa katika idadi ya michango kati ya wabunge waliorudi na wale ambao hawakurudi. Wabunge 55 wa CCM waliorudi walichangia wastani mara 83...
"Ambapo wabunge wa CCM 108 ambao hawakurudi walichangia kwa wastani wa mara 80. Wabunge 3 wa CHADEMA waliorudi walichangia hoja kwa wastani wa mara 174, ambapo wabunge 2 ambao hawakurudi walichangia hoja mara 173.".
Chama kilichokuwa na wabunge wenye ushiriki mdogo bungeni kilipoteza viti katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010, ambapo utafiti huo umeonesha kuwa wabunge wa CUF na CCM kwa kiasi fulani walikuwa na ushiriki mdogo, ambapo wale wa CUF walichangia mara 87 na wabunge wa CCM walichangia kwa wastani michango 80.
Utafiti huo umesema kuwa chama kilichokuwa na wabunge wenye ushiriki mkubwa bungeni katika bunge la tisa kilifanikiwa kuongeza viti katika uchaguzi mkuu uliopita, ambapo wabunge wa kawaida wa CHADEMA, ndiyo waliochangia zaidi kwa wastani wa hoja mara 173.
"Chama kilichotoa michango mingi bungeni (CHADEMA), kiliongeza asilimia ya wabunge kwa zaidi ya mara nne, kutoka asilimia 2 mpaka 9. Kwa upande mwingine chama chenye ushiriki mdogo zaidi (CCM) kilipunguza asilimia 89 hadi 78.
"CUF chama ambacho kilikuwa na ushiriki zaidi ya ule wa wabunge wa CCM, kiliongeza kidogo asilimia yake ya wabunge kutoka asilimia 8 hadi 10. Matokeo haya yanaelekea kukubaliana na maoni kwamba wapiga kura wanazingatia kiwango cha ushiriki wa wabunge wakiwa bungeni, wakati wanapoamua chama kipi wakipigie kura."
No comments:
Post a Comment