19 April 2011

Viongozi Simba 'kuteta' kesho

Na Elizabeth Mayemba

KAMATI ya Utendaji ya Simba, inatarajiwa kukutana kesho kwa ajili ya kupanga terehe ya Mkutano Mkuu wa wanachama, pamoja na kujadili suala la usajili kwa
wachezaji watakaoachwa na wapya.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Msemaji wa klabu hiyo, Cliford Ndimbo alisema kamati hiyo itakutana kesho baada ya Kamati ya Ufundi kumaliza kikao chake na kutoa maamuzi yao.

"Kesho ndiyo Kamati ya Utendaji itakaa na kupitia mambo mbalimbali ya usajili wa wachezaji wapya na wale watakaoachwa, pia watapanga na siku ya Mkutano Mkuu wa wanachama wa kila mwaka," alisema Ndimbo.

Alisema katika suala la usajili, kuna wachezaji ambao wameshapata timu nyingine hivyo watatakiwa kuongezwa wengine na pia wapo watakaotemwa, hivyo kamati itapitia ili kuweka hadharani kila kitu.

Ndimbo alisema wiki iliyopita, Kamati ya Ufundi ilikutana kwa ajili ya kujadili mambo mbalimbali pamoja na kupitia ripoti ya Kocha Mkuu Patrick Phiri, hivyo kuna maamuzi ambayo yalifikiwa na kuyapeleka kwenye Kamati ya Utendaji ambayo nayo itapitia kila kitu kesho na kutolea maamuzi.

Alisema baada ya kikao hicho, klabu hiyo itaelekeza nguvu katika michuano ya Kombe la Kagame inayotarajiwa kuanza Julai 5 mwaka huu, nchini Sudan.

Tayari Simba imeshaondokewa na wachezaji wake nyota watatu, Mbwana Sammata na Patrick Ochan waliopata ulaji TP Mazembe ya Congo DRC na Emmanuel OKwi ambaye ameitwa kufanya majaribio Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment