Na Raphel Okello-Bunda
MWENYEKITI wa Mamlaka wa Mji wa Bunda, Bw. Pastory Ncheye amewataka wananchi wa mji huo kuwa na subiri katika kesi inayomkabili katika Mahakama ya
Wilaya ya Bunda kwa tuhuma ya kutoa rushwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010.
Akizungumza na baadhi ya wananchi hao baada ya kesi yake kutajwa katika mahakama hiyo, Bw. Ncheye alisema kwa kuwa jambo hilo limeshafikishwa mahakamani hawezi kusema chochote badala yake anaichia mahakama, ingawa alidai kuwa ni kesi iliyopikwa na baaadhi ya vigogo wa kisiasa.
Kesi hiyo ya kutoa rushwa wakati wa uchaguzi inayomkabili Bw. Ncheye iliahirishwa jana baada ya kutokuwepo kwa hakimu anayesikiliza kesi hiyo.
Uamuzi wa kuahirisha kesi hadi Mei 30, mwaka huu ulitolewa na Hakimu wa Wilaya ya Bunda, Bw. James Manota kwa niaba ya Hakimu Mfawidhi, Bi. Safina Simfukwe.
Kwa mara ya kwanza Bw. Ncheye alifikishwa mahakamani hapo Februari 28, mwaka huu ambapo Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) wilayani Bunda, Bw. Erick Kiwiya alimsomea mashtaka matatu ikiwa ni pamoja tuhuma ya kutoa rushwa ya sh. 20,000 kwa mabalozi watatu wa mashina wa CCM ili wamfanyie kampeni ya kushinda kiti cha udiwani wa kata ya Bunda mjini katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.
Kwa mjibu wa Bw. Kiwiya alidai Bw. Ncheye alienda kinyume na kifungu namba 6 cha Sheria ya Gharama za Uchaguzi ya mwaka jana, na Bw. Ncheye alikanusha tuhuma hizo.
No comments:
Post a Comment