19 April 2011

TBL yamwaga 'minoti' mikoani

Na Zahoro Mlanzi

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Kilimanjaro Lager, imetoa sh. milioni 375 kwa ajili maandalizi ya mikoa itakayoshiriki mashindano ya Kombe la
Taifa (Kili Taifa Cup) mwaka huu.

Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza kutimua vumbi Mei 7, mwaka huu katika vituo sita na hatua ya robo, nusu na fainali zikitarajiwa kufanyikia kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Akizungumza wakati wa semina kwa waandishi wa habari iliyofanyika mwishoni mwa wiki, Meneja wa bia ya Kilimanjaro, George Kavishe alisema katika mashindano ya mwaka huu wataanzia ngazi ya mikoa, kanda na baadaye taifa.

"Hatutaweza kuanza katika ngazi ya awali kabisa kama tulivyosema awali kutokana na uwezo tuliokuwa nao, hivyo Taifa Cup itaanzia mikoani ambapo nina imani tunaweza kupata vipaji kuanzia hapo," alisema Kavishe.

Alisema katika kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa kwenye mashindano hayo, wameanza kutoa fedha kwa ajili ya mikoa shiriki ambapo kila mkoa utapata sh. milioni 1.5 kwa ajili ya gharama mbalimbali ili timu zifike katika kituo husika.

Kavishe alisema inawezekana hizo fedha za maandalizi zikawa hazitoshi ndiyo maana huwaagiza Wakuu wa Mikoa, kufanya jitihada zingine ili kuhakikisha timu zao zinapata mahitaji yanayotakiwa.

"Huo utaratibu wa kutoa fedha kwa mikoa limeshaanza na tunatarajia mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi huu, kila mkoa uwe umeshapata fedha zake na kila mkoa utakuwa na watu 25," alisema Kavishe.

Aliitaja mikoa ambayo itatumika kama vituo vya mechi za awali katika makundi ni Kilimanjaro, ambao utakuwa na timu za Arusha, Tanga, wenyeji wenyewe na timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 23.

Kituo kingine ni Mwanza kitakachokuwa na timu za Mwanza, Mara, Kagera na Shinyanga, kituo cha Tabora kina timu za Tabora, Kigoma, Singida na Dodoma na kituo cha Mbeya kina timu za Rukwa, Mbeya, Iringa na Temeke.

Vituo vingine ni Mtwara kina timu za Mtwara, Ruvuma, Kinondoni na Lindi na kituo cha mwisho ni Morogoro chenye timu za Pwani, Manyara, Ilala na Morogoro.

No comments:

Post a Comment