11 April 2011

Vibali kwenda kwa Babu vyasitishwa Bunda

Na Raphael Okello, Bunda

SIKU mbili baada ya wagonjwa wanaokwenda kwa Babu Loliondo kufunga barabara juzi katika kituo cha Bunda mkoani Mara kulalamikia ucheleweshaji katika
kituo hicho, serikali imesitisha usajili na utoaji wa vibali kwa siku mbili.

Mkuu wa mkoa wa Mara, Bw. Enos Mfuru juzi aliagiza vibali kusitishwa kwa muda kusubiri utararibu mwingine wa serikali kwa madai kuwa kituo hicho kimezidiwa, hali iliyozidisha msongamano katika kituo hicho.

Jana hakuna magari yaliyosajiliwa katika kituo hicho licha ya magari mengi kumiminika kuingia kituoni hapo kwa siku za wikiendi huku habari zaidi ambazo hazikuthibitishwa na serikali wilayani humo zikieleza kuwa mgonjwa mmoja kutoka Kigoma amepoteza maisha akiwa kituoni hapo.

Wakati magari kutoka nje ya wilaya hiyo na wagonjwa wao  wakiendelea kusota kituoni hapo, wanaokata tiketi ya magari yanayomilikiwa na wenyeji wa Bunda wameendelea kusafirisha wageni kwenda Loliondo huku maswali mengi yakiulizwa ni wapi wanakopata vibali hivyo.

Kutokana na magari ya Bunda kuonekana kupata vibali kwa haraka, jana mwandishi wa habari hizi alishuhudia baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wakiwapigia simu wenzao ambao hawajafika kituoni hapo kuwataka kutokata tiketi ya magari ya nje, badala yake waende hadi Bunda ili kupata tiketi ya magari ya wenyeji wa mji huo ambao yanadaiwa kupata vibali kwa haraka.

“Ninachoweza kusema ni kwamba tiba hii ya Babu sasa imekuwa mtaji kwa watendaji wa serikali kwa sababu fedha sasa zinatumika sana katika safari hii ya kwenda Loliondo kwani unalazimika kutoa rushwa ili upate vibali,” alilalamika mmoja wa wagonjwa.

Awali Mkuu wa Wilaya ya Bunda Bw. Francis Isaac
alibaini kuwepo kwa vibali visivyotolewa na ofisi yake ambavyo vinatumiwa na baadhi ya wamiliki wa magari kwenda Loliondo ambapo alitoa tahadhari dhidi ya wanaogushi vibali hivyo.

1 comment:

  1. Hivi hao wanaopokea rushwa hawaogopi! Kwani babu akifanya maombi wanaweza kuwa maskini zaidi au wakapoteza uwezo wa kuona-upofu, kama yule jamaa mwizi wa pochi.
    Dah yani watanzania wengine wamekosa huruma kabisa, wamefanya safari ya kwa babu dili sasa, hadi watu wengine wanapoteza maisha hata kabla ya kumuona huyo babu. Inatupasa kubadilika na kuwa na moyo wa Huruma.
    Mwasheni N

    ReplyDelete