Na Rashid Mkwinda, Mbeya
TAFRANI iliibuka mwishoni mwa wiki katika mji mdogo wa Uyole baada ya nyumba ya kiongozi wa kabila la Wasafwa, Chifu Paulo Mwanshinga kubomolea na
mfanyabiashara maarufu wa mjini Tunduma, Bw. Saliwe Sanga aliyedaiwa kununua eneo hilo kwa sh. milioni 18.
Chifu Mwanshinga ambaye kwa sasa ni marehemu alikuwa ni kiongozi wa kabila la Wasafwa kabla ya kifo chake miaka kadhaa iliyopita ambapo nyumba hiyo Kitalu namba A 50 kiwanja namba 85 yenye thamani ya sh. milioni 200 iliendelea kubaki chini ya wanafamilia wakiitunza na kuienzi kulingana na maagizo ya kiongozi huyo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafamilia, mmoja wa wanafamilia Bi. Grina Mwanshinga alisema kuwa nyumba hiyo ni ya wanafamilia ambayo pia ilikuwa ikitumiwa kwa ajili ya shughuli za mila na desturi za kabila hilo.
Alisema kuwa hata hivyo uuzaji huo unaonekana kama ni wa kitapeli kwa kuwa hata muuzaji aliyemtaja kwa jina la Eliofoo Mwanshinga hajulikani alipo na kwamba kitendo cha kuanza kubomolewa nyumba hiyo ni sawa na uvamizi.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Itezi iliko nyumba hiyo, Bw. Peter Lingo alisema kuwa kilichofanyika ni uvamizi na kwamba mara baada ya wanafamilia hao kuona ujenzi unaendelea katika eneo hilo, walifika na kuzuia ujenzi uliokuwa ukiendeshwa na mfanyabiashara huyo.
Baada ya wanafamilia kuzuia ujenzi, mnunuzi wa eneo hilo Bw. Sanga alifika na kueleza kuwa yeye amenunua eneo hilo kihalali na atendeleza ujenzi huo, hali ambayo iliibua mvutano baina ya pande hizo.
Bw.Sanga alisema kuwa yeye amefuata taratibu zote za ununuzi wa kiwanja hicho na kwamba kilichofanywa na wanafamilia hayo ni sawa na kumfanyia vurugu katika haki yake.
Alisema kuwa iwapo anaonekana amekwenda kinyume katika taratibu za ununuzi wa nyumba hiyo, wanafamilia hao wanaweza kufuata mkondo wa sheria ikiwa ni pamoja na kwenda mahakamani.
Kitendo hicho kiliibua tafrani katika eneo hilo la ujenzi hali iliyosababisha Askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) kuwasili eneo hilo la tukio na kuwachukua wanafamilia hao hadi Kituo Kikuu cha Polisi jijini Mbeya na kufunguliwa jalada la kufanya vurugu.
Wanafamilia waliodaiwa kufanya vurugu eneo hilo ambao ni Bi. Grina Mwanshinga, Bw.Patson Mwanshinga, Bw. Mwalizi Mwanshinga, Bw. Benjamin Mwanshinga na kiongozi wa machifu Bw. Roket Mwanshinga namba IR/RB/3191/2011.
Mkuu wa Machifu wa kabila hilo, Mwene Roketi Mwanshinga alisema kuwa, ndani ya nyumba hiyo kulikuwa na chumba maalumu kilichokuwa kikitumika kwa matambiko ya mila na desturi za kabila lao.
Alisema ili kurejesha hali ya usalama katika mji huo inatakiwa kutolewa kafara ya kuchinjwa ng’ombe, mbuzi, kondoo na kuku, vinginevyo linaweza kutokea jambo lenye madhara juu ya mvamizi wa eneo hilo.
Mbali na kushikilizwa kwa wanafamilia hao kwa saa nne kuanzia saa 10:00 jioni hadi saa 2:00 usiku, imedaiwa kuna maagizo kutoka ndani ya jeshi la polisi kuzuia kuendelea na ujenzi huo.
Pande hizo mbili zinazovutana zikutanishwe na upande wa tatu (Mediator)yaweza kuwa hata ni Jeshi la Polisi na hapo utolewe ufafanuzi wa kisheria kuhusu suala hilo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake kwa Amani na Maridhiano.Maana kuuza & kununua linapaswa kuwa ni suala la makubaliano ya pande mbili i.e Muuzaji & Mnunuzi.
ReplyDeletePascal Mwalyenga - NGARA KGR.
Hivi hadi hii leo bado kuna matambiko tu! yanafanya kazi kweli? au kupoteza muda tu!
ReplyDeletemh inaonekana kuna dalili zote za utapeli,kwani hichi kiwanja kilitakiwa kiuzwe baada ya familia kurithia sasa inaonekana mmoja kati ya wanafamilia amewazunguka wenzake. jambo la muhimu ni huyo sanga kukaa na wanafamilia kuangalia wanafanya nini la sivyo yanaweza yakatokea maafa ambayo yanaweza kuepukika.
ReplyDeleteMwashitende N