LONDON, England
MCHEZAJI Salomon Kalou ameelezea furaha yake isiyo kifani, baada ya timu yake ya Chelsea kurejea kwenye kiwango chake na kuibuka na ushindi wa mabao
3-1, dhidi ya West Bromwich Albion katika mchezo uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita.
Wiki iliyopita, Blues ilitupwa nje ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya na Manchester United, lakini katika mchezo huo ikabadilika na kuonesha kiwango kikubwa dhidi ya timu hiyo ya Baggies na kuifanya Chelsea ibakishe pengo la pointi mbili dhidi ya Arsenal iliyopo nafasi ya pili.
Katika mechi hiyo Kalou, ndiye aliyepachika bao la pili lililoifanya Chelsea, iwe mbele baada ya kusawazisha awali na akasema anaona fahari kubwa kuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji wenzake walioonesha uwezo huo.
“Tulicheza vizuri kipindi cha kwanza, tulicheza vizuri sana wakati tukiwa nyuma kwa bao 1-0,” Kalou aliiambia tovuti ya klabu. “Huo ndiyo moyo ambao kila mmoja alikuwa akihitaji kuuona Chelsea ina upinzani mzuri, baada ya kutoka kwenye kipigo cha kutolewa nje ya michuano ya Klabu Bingwa," aliongeza.
Alisema ulikuwa ni upinzani mzuri kwani baada ya kupatikana goli, kila mmoja alipigana ingawa awali ilionekana itakuwa mechi nyingine ngumu kwa Chelsea, lakini vijana wakaungana pamoja na kufanya kazi kubwa na akasema anahisi hicho ndicho kiwango cha timu.
No comments:
Post a Comment