Na Zahoro Mlanzi
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limesema usajili wa wachezaji kwa ajili ya mashindano ya Kombe la Taifa 'Kili Taifa Cup', utaanza Aprili 26, mwaka
huu kwa mikoa yote.
Mashindano hayo yanatarajia kuanza kutimua vumbi katika vituo sita vya mikoa mbalimbali nchini kuanzia Mei 7, mwaka huu ambayo yameandaliwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia yake ya Kilimanjaro Lager.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema Mei 2 ndiyo siku ya mwisho kwa mikoa kuweka pingamizi ambapo baada ya hapo Kamati ya Mashindano hayo, itakutana siku inayofuata.
"Mei 5 tunatarajia timu za mikoa kuanza safari ya kwenda vituoni tayari kwa mashindano na tuna imani fedha za maandalizi zitakuwa zimewafikia kwani wadhamini TBL, walishaanza kuzitoa," alisema Wambura.
Wakati huo huo, Wambura alisema Shirikisho la Mpira wa Miguu la Afrika (CAF), limeteua waaamuzi sita nchini kwenda kuchezesha michezo ya awali ya michezo ya Afrika (All African Games), katika nchi mbalimbali zinazowania kufuzu michezo hiyo.
Aliwataja waamuzi hao kuwa ni Waziri Sheha, John Kanyenye na Hamisi Chang'walu ambao watakwenda kuchezesha mchezo kati ya Malawi na Afrika Kusini utakaopigwa jijini Lilongwe Aprili 30, mwaka huu.
Wengine ni kwa upande wanawake ambapo Judith Gamba, Saada Hussein na Mwanahija Makame wao watakwenda nchini Zimbabwe kuchezesha mchezo kati ya timu ya taifa ya nchi hiyo, itakayoumana na Angola katika mchezo utakaopigwa Mei 14, mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Wambura alisema timu ya Gaborrone United inahitaji kocha wa kuifundisha timu hiyo kutoka nchini ambapo mwenye sifa anatakiwa awasiliane na TFF, ili kujua taratibu za kufuata.
No comments:
Post a Comment