20 April 2011

Ukuta waua watoto wanne

Na Masau Bwire

WATOTO wanne waliokuwa wakisoma katika Shule ya Chekechea ya Nia iliyopo Kimara B, Matosa, Kinondoni jijini Dar es Salaam wamekufa na wengine watatu
kujeruhiwa vibaya baada ya kuangukiwa na ukuta.

Tukio hilo limetokea jana saa 6.30 mchana baada ya ukuta wa nyumba jirani na shule hiyo kuwaangukia watoto hao waliokuwa wakicheza kwenye bembea.

Jeshi la Polisi wilaya ya kipolisi Kimara liliwataja watoto waliokufa ambao miili yao imehifadhiwa katika Hospitali Teule ya Tumbi kuwa ni Gladness Shimwela (5), Devotha Living (5), Ludatrice Lawrence (3) na Isaack Ndosi (5).

Watoto waliojeruhiwa walitajwa kuwa ni Angela Jonas (5), Asumwene Uswege (5) na Lilian Dominick (3) ambao wote wamelazwa katika Hospitali ya Tumbi.

Taarifa kutoka jeshi la polisi zilisema, mmiliki wa ukuta huo Bw. Amani Mashika ambaye hakuwepo wakati ukuta huo unaanguka bado hajapatikana ili kueleza nini hasa chanzo cha ukuta huo kuanguka.

Aidha jitihada za mwandishi wa habari hizi kuupata uongozi wa shule hiyo inayomilikiwa na mke wa Profesa Philemon Sarungi, Bi. Jackline Sarungi hazikufanikiwa kwa kuwa walikuwa wakishughulikia kutoa huduma kwa majeruhi ili kuwawahisha hospitalini.

2 comments:

  1. Vifo vya watoto hao havitakuwa bure kama wahusika watawajibishwa na wajenzi wengine watajifunza somo la usalama.

    ReplyDelete
  2. Chanzo cha kuanguka ukuta kinajulikana. Inachotakiwa ni mwenye ukuta awajibishwe. Ikiwezekana alipe fidia kwa walioathirika na uzembe huo. Mwenye shule pia yampasa kuwajibika kwani alirushusu watoto kuchezea sehemu isiyo salama. Wajibu wa mwenye shule unaisha pale anapomkabidhi mtoto kwa mzazi au mlezi wake. Siasa haitakiwi hapa, inabidi sheria ifuatiliwe ipasavyo, la sivyo nchi hii itakuwa imeoza.

    ReplyDelete