20 April 2011

Serikali yazuia ujenzi Kipunguni

Na Heri Shaaban

SERIKALI imelazimika kuingilia kati sakata la mgogoro wa ardhi katika Kata ya Kivule eneo la Kipunguni B Manispaa ya Ilala kwa kuwazuia wakazi wa eneo hilo wasiendeleze
ujenzi wa aina yoyote kwa kuwa litatumika kwa shughuli nyingine za kijamii.

Kutokana na amri hiyo wakazi wa eneo hilo waliojenga wametakiwa kubomoa na wale wanaouza maeneo waache mara moja.

Tamko hilo lilitolewa Dar es Salaam jana na Meya wa Manispaa Ilala, Bw. Jerry Silaa wakati akihutubia mkutano wa wakazi wa eneo hilo, wakati wa kusuluhisha mgogoro wa Ardhi.

Bw. Silaa alisema kuwa alipokea malalamiko ya watu kugombea eneo kutokana na kuuziana kinyemela, kwa kushirikiana na ofisi ya mkurugenzi wakaafikiana kutoa agizo hilo.

"Ardhi ni mali ya Serikali hakuna mtu mwenye ardhi yake, ndio maana tumezuia ujenzi usiendelee ili kuzuia umwagaji wa damu au machafuko na mtu anayedai eneo hilo la wazi la kwake awasiliane na ofisi ya Kata kwa maelezo na vithibitisho," alisema Bw. Silaa.

Meya huyo alisema kuwa kila jambo lina wakati wake, Ilala ina eneo kubwa la ardhi ambalo halijapimwa na kila ardhi iliyopo Dar es Salaam ina mwenyewe.

Aliwataka wakazi wa eneo hilo waliokuwa wakitishiana kwa silaha na kuuziana kinyemela kuacha kufanya hivyo kwa kuwa mpaka sasa eneo hilo linamilikiwa na halmashauri hiyo.

Alisema kuwa mapendekezo ya kikao cha kata ni kuwa eneo hilo lijengwe shule na huduma zingine ambazo hazipo.

No comments:

Post a Comment