*Asema ni majigambo ya kisiasa yasiyo na manufaa
*Mukama asisitiza walichofanya si nguvu ya soda
Na Grace Michael
MABADILIKO ya kujivua gamba yaliyofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuibua mjadala katika jamii na
vyombo vya habari yameelezwa kutokuwa na maana kwa kuwa hayana mkakati wowote wa kuondoa umasikini unaowakabili wananchi kwa sasa.
Kutokana na hali hiyo, CCM kimetakiwa kuachana na majigambo ya kisiasa na badala yake kije na mkakati wa kuwaondoa wananchi katika ugumu wa maisha unaowakabili kwa sasa.
CCM kilifanya mabadiliko ya uongozi wake wa ngazi ya juu ambayo ilitanguliwa na kujiuzulu kwa sekretarieti nzima ya chama hicho na Kamati Kuu na kuteua wajumbe wengine, akiwamo Katibu Mkuu mpya, Bw. Wilson Mukama.
Pamoja na kufanyika kwa mabadiliko hayo ambayo wana-CCM wanaeleza kwamba yatasaidia kurejesha heshima ya chama hicho kwa jamii na kutoa tambo kwa vyama vya upinzani kuwa kimejipanga upya kupambana nao baada ya kuwatoa wale kinaodai ni mafisadi.
Hata hivyo, kadri siku zinavyokwenda, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wameanza kuukosoa mkakati huo, wakisema unatakimaliza zaidi kwa kuwa kitakuwa na mgawanyiko mkubwa huku Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi Bw. James Mbatia akisema wazi kuwa hayana tija kwa kuwa wananchi wako katika hali ngumu kimaisha.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Bw. Mbatia alisema kuwa kinachotakiwa kwa sasa ni kujadili namna ya kuwaondoa wananchi katika umaskini mkubwa unaowakabili na si mambo ya kutambiana au kukabiliana kisiasa.
"Jamani namuomba Mukama ambaye ni Katibu Mkuu wa CCM na vyama vyote vya siasa kuachana na malumbano ya kisiasa na badala yake tujadili mambo yanayowakabili wananchi...daraja la wenye nacho na wasio nacho limekuwa kubwa, mifumko ya bei, maisha yamekuwa magumu kwa wananchi hivyo mambo ya kujigamba kuikabili CHADEMA au wapinzani, hayana tija tuangalie namna ya kuwakomboa wananchi hapa walipo," alisema Bw. Mbatia.
Alisema kuwa nchi ina mambo mengi ya kujadili ili kukabiliana na umasikini unaoongezeka kila kukicha ambapo shilingi ya Tanzania nayo inazidi kushuka thamani yake dhidi ya dola, hivyo CCM badala ya kujigamba kuvua magamba wanatakiwa kuja na mkakati wa kumaliza matatizo hayo ambayo ndiyo kero kubwa kwa wananchi.
Kutokana na hayo, Bw. Mbatia alisema kuwa hoja zote zinazotolewa na viongozi wapya wa CCM akiwemo Bw. Mukama ambaye ameweka wazi msimamo wake kuwa mabadiliko hayo si nguvu ya soda, ni hoja nyepesi zisizo na mashiko kwa kuwa haziwasaidii wananchi kuondokana na umaskini.
"Mwaka 2015 Tanzania tutahukumiwa na malengo ya milenia kwa kuwa tutatakiwa kueleza tumeyatekelezaje na malengo hayo ni kuondokana na umasikini, elimu kwa wote, usawa wa kijinsia na kuwawezesha akina mama, kupunguza vifo vya watoto wenye umri wa chini miaka mitano na vifo vya akina mama wajawazito, kupambana na UKIMWI na ushirikishanaji," alisema Bw. Mbatia.
Kuvua gamba si nguvu ya soda
Katika hatua nyingine, Mwajuma Juma anaripoti kutoka Zanzibar kuwa Bw. Mukama amesema kuwa moto uliowashwa na chama hicho hivi karibuni kuhusiana na mafisadi ndani yake umelenga katika kurejesha imani kwa wananchi wakione kuwa ni chama bora na sio nguvu ya soda.
Kauli hiyo ameitowa huko katika Ofisi Kuu ya Chama hicho Kisiwandui mjini Unguja wakati akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wazee, ikiwa ni mfululizo wa utambulisho wa wajumbe wa Sekretarieti mpya iliyoteuliwa baada ya ile ya awali kujiuzulu.
Alisema kuwa moto huo haukuwa nguvu za soda na wala hautazimika hadi pale wananchi watakapokiamini na kuona kuwa ndio chama pekee ambacho kitakuwa ni kimbilio la wanyonge badala ya kuwa matajiri.
Alifahamisha kuwa ili kufikia azma hiyo chama hicho kwa sasa kimejipanga vizuri kwa kubuni mbinu mbalimbali na mikakati madhubuti, ambayo itasaidia kurejesha haiba yake iliyopotea miongoni mwa wananchi.
“Moto uliowashwa ndani ya chama hichi siyo nguvu za soda na hautazimika hadi imani ya wananchi dhidi ya chama iweze kurejea kwa Watanzania wote,” alisema.
Katika kikao hicho, wazee hao walitoa shukrani zao kwa viongozi hao kwa hatua waliyofikia na kuwataka viongozi wa mikoa hadi taifa kuungana ili agizo la katibu huyo liweze kufikiwa.
Bw. Mukama yupo Zanzibar kwa ajili ya kuwatambulisha wajumbe wa Sekretarieti ya NEC, tangu Aprili 17, mwaka huu.
Ripoti ya CAG na NCCR
Bw. Mbatia alitumia mwanya huo kumtaka Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Bw. John Tendwa kukisafisha chama hicho na tuhuma za kushindwa kuwasilisha hesabu za matumizi ya fedha za ruzuku kwa madai kuwa NCCR-Mageuzi kimewasilisha ripoti ya ukaguzi katika ofisi yake.
Bw. Mbatia alisema kuwa chama chake kimekuwa kikitekeleza sheria ya vyama vya siasa inayotaka kukaguliwa kwa fedha zake kila mwaka ambapo alionesha ripoti ya ukaguzi kuanzia mwaka 2005 hadi sasa.
Alisema kuwa ni haki ya wananchi kujua namna ya fedha za ruzuku zinavyotumika na ndio maana chama hicho kinatekeleza sheria hiyo kwa kukaguliwa fedha za ruzuku pamoja na fedha za vyanzo vingine kama ada za wanachama.
"Hizi taarifa za ufisadi wa fedha za ruzuku kwa vyama vya siasa zimeleta mtafaruku mkubwa kwa kuwa wanachama wengi wanapiga simu wakihoji kuhusu suala hili na wanafanya hivyo kwa kuwa chama kimeweka utaratibu wa kuweka wazi mapato na matumizi, hivyo tunamwomba msajili atusafishe kwa kuwa nakala ya ripoti ya ukaguzi anayo," alisema Bw. Mbatia.
Alisema NCCR-Mageuzi hakiko kwenye kundi la ufisadi wa fedha za walipa kodi kwa kuwa kila mwaka hukaguliwa na ripoti kuwasilishwa katika mamlaka husika.
Bravoo Mbatia,malumbano hayasaidii,wananchi wanateseka wao wanasiasa wananeemeka
ReplyDeleteMukama mbona hatujasikia mkitaja majina ya mafisadi kama mna nia kweli ya kupambana na ufisadi ndani ya chama tajeni majina ya hao mafisadi hadharani. vinginevyo ni usanii mtupu.
ReplyDeleteccm mmekuwa wasaanii, mnapiga kelele ili msikike lakini mkisikika hamna cha maana kinaeleweka kutoka kwenu. Kama wajasiri kweli mnashindwa nini kuwataja hao mafisadi? Wenzenu mbona wanataja? Mkama na genge lako mtajikuta mnashindwa kujibu maswali ya wananchi mkiendelea na kelele zenu.
ReplyDeleteCha msingi kaeni chini mje na mpango mkakati wa kuwapa vijana ajira, kuwa na mipango ya kuzuia wageni kupora ajira za vijana kwa kuwabana wageni watoe ujuzi na kuondoka sio kufanya hata na kazi za uhasibu. Wageni wamejaa humu nchini wanachukua ajira zetu mnasikiaaaaaaaaaaaaaaaa
Huu wa CCM ni usanii mtupu. Wananchi tunataka mabadiliko ya kweli haswa hali ya maisha. Inashangaza hawa wakina Nape wanazunguka na kufanya mikutano ya hadhara hawasemi mikakati ya kumkomboa Mtanzania ni ipi maana wao ndio wanajisifia CCM imejivua gamba. Mbona mapambano yao ni dhidi ya CHADEMA tu sisi hayo yanatusaidia nini jamani? Inaelekea hofu yao ni kupata madaraka ili waidhibiti CHADEMA na sio kuwasaidia walalahoi. Hawatafanya lolote la maana sana sana wanazidisha mpasuko ndani ya CCM na kujijengea maadui.
ReplyDelete