21 April 2011

UDOM wagoma, waandamana kwa Pinda

Na Pendo Mtibuche, Dodoma

WANAFUNZI wa Chuo cha Sayansi ya Kompyuta na Mawasiliano (UDOM) jana waligoma kuingia madarasani na kufanya maandamano hadi Ofisi ya
Waziri Mkuu lengo la kufikisha madai yao hasa ya fedha za  mafunzo kwa vitendo kutoka Bodi ya Mikopo.

Miongoni mwa wanafunzi hao ambao walizungumzia suala hilo walisema kuwa hawaridhiki na kiasi ambacho Bodi ya Mikopo ilichopendekeza cha sh. 350,000 badala ya sh. 850,000 ambazo wanafunzi hao walipendekeza kwa bodi hiyo.

Elias Lugwisha alisema awali wanafunzi hao walipeleka mapendekezo ya fedha zinazohitajika katika Bodi Mikopo kwa mujibu wa mahitaji ya kozi yao ambapo alisema kuwa waliwaomba sh. 850,000 kwa ajili ya kununulia vifaa vya kujifunzia ikiwemo kompyuta"

Hata hivyo, alisema kuwa baada ya muda Bodi ya Mikopo waliwajibu  kuwa watawalipa kiasi cha sh. 350,000 badala ya 850,000 kama walivyopendekeza, hali ambayo alisema kuwa kiasi cha sh. 350,000 ni kidogo kulingana na hali halisi ya mafunzo kwa vitendo.

Alisema kuwa kitendo cha kupewa mkopo wa sh. 350,000 ambao wengi wao hawakuridhika nacho ndiyo sababu ya kugoma kuingia madarasani na kuamua kufanya maandamano hadi Ofisi ya Waziri Mkuu ili kufikisha kilio chao.

Alibainisha kuwa kabla ya maandamano hayo kufanyika watu kutoka Bodi ya Mikopo walifika chuoni hapo na kutoa majina ya wanafunzi waliodai kuwa ndio waliokubaliwa kupewa mkopo huo ambapo majina ya wanafunzi wa mwaka wa tatu hayakuwepo.

Kwa mujibu wa Lugwisha wanafunzi wengine walilipwa sh. 50,000, wengine 70,000 na wengine 120,000, jambo ambalo pia limesababisha wamefikie maamuzi ya kugomea fedha hizo na kuandamana.

Kwa upande wake Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Bw. Gerald Guninita akizungumzia tukio hilo katika ofisi hizo alisema kuwa wanafunzi hao wanapaswa kurudi chuoni wakati jitihada za kutatua matatizo yao zikifanyika.

Vile vile alisema tayari taarifa hizo Waziri Mkuu ameshapatiwa  hivyo aliwasihi wanafunzi hao kuwa wasubiri jibu lao mapema Mei 6, mwaka huu hivyo kwa wakati huu wanafunzi hao waendeleo kuwa wavumilivu.

1 comment:

  1. hawa wa2 wa mawasiliano hawano solidarity,ndo mama wenzao wamewachunia watalimaliza wenyewe

    ReplyDelete