21 April 2011

Maelfu kusota pasaka na Babu

Na Said Njuki, Arusha

ZAIDI ya wagonjwa na ndugu 3,000 watalazimika kusherehekea Mateso, Kufa na Kufufuka kwa Yesu Kristo (PASAKA) na Mchungaji Ambilikile Masapila, wakisubiri
kupata kikombe atakapoanza huduma Jumanne ijayo.

Wananchi hao wamefikia hatua ya kukaa katika Kijiji cha Samunge Wilayani Ngorongoro baada ya kushindwa kumfikia 'Babu' kabla ya sikukuu hiyo kuanza leo.

Habari kutoka Kijiji cha Samunge zilidai hakuna uwezekano wa Babu kuvuta msururu mrefu unaokadiriwa kufikia kilomita 25 kutoka kwake kwa jana na leo.

Ilielezwa kuwa wagonjwa ambao hawatafanikiwa kupata kikombe hicho kati ya jana na leo watalazimika kusubiri hadi sikukuu hizo zipite kwa kuwa Babu alishatangaza mapema kupumzika siku hizo.

“Ukweli ni kwamba hakuna mgonjwa hata mmoja atakayerudi nyumbani baada ya kufika Samunge baada ya babu kusitisha tiba hiyo kusherehekea Siku ya PASAKA.

Naamini wote waliofika hapa watalazimika kusubiri hadi Jumanne ijayo atakaporudi kazini babu,” alisema Bw. Abdulrahman kutoka Samunge.

Alisema msururu wa magari bado unaongezeka licha ya serikali kutoa taarifu kuzuia wagonjwa na wasindikizaji kutosafiri tena kuelekea Samunge kutokana na Babu kupanga kupumzika.

Mkuu wa Wilaya Bunda mkoani Mara, Bw. Francis Issack, alisema jana kuwa tangu juzi wameanza kuzuia magari yasiende kwa Mchungaji Masapila kutokana na msongamano.

“Jana (juzi) kulikuwa na gari kadhaa tulizizuia na hata leo (jana) hakuna ruhusa ya gari kuelekea huko,” alisema Bw. Issack.

Hata hivyo habari kutoka Babati na Arusha mjini zinaeleza kuwa bado watu walikuwa njiani kuelekea Samunge licha ya agizo hilo la serikali.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Bw. Elias Lali, alisema hali bado ni mbaya na uwezekano wa babu kumaliza idadi ya wagonjwa waliofurika katika kijiji hicho kabla ya Siku ya Ijumaa Kuu ni ndogo.

Alisema kuna uwezekano mkubwa wa wagonjwa hao kushirikiana na Babu kula sikuu ya PASAKA wakisubiri tiba baada ya mapumziko hayo.

"Ndiyo kwanza naelekea huko lakini nikuhakikishie ndugu yangu, uwezekano wa mchungaji kumaliza idadi kubwa ya wagonjwa waliofurika huko kwa muda huu uliobaki ni ngumu.Labda watalazimika kula siku hizo na babu huku wakisubiria siku hizo zifika wapate tiba ndio waondoke,” alisema.

Hata hivyo serikali ndio inayolaumiwa kwa kushindwa kudhibiti mapema idadi ya watu kwa kuwa Mchungaji Masapila alitoa ratiba ya kupumzika PASAKA muda mrefu.

Baadhi ya wananchi Mkoani Mara na Babati walidai baadhi ya watendaji wa serikali wameshiriki kuongeza adha kwa wagonjwa kwa kutoa vibali na kuwaruhusu kuanza safari badala ya kuchukua hatua mapema kulingana na tangazo la Babu.

Katika hatua nyingine wagaonwja hao na ndugu zao wanakabiliwa na hali ugumu ya maisha kutokana na bei za vyakula na bidhaa zingine kuendelea kupaa kwa zaidi ya mara mbili.

Habari zilizolifikia gazeti hili zilieleza kuwa chakula cha bei ya chini ambacho ni ugali ama wali maharage inauzwa kati ya sh 2,500 na 3,500.Maji ya kunywa nusu lita inauzwa sh. 1,000 huku lita moja ikiuzwa sh. 2,000.Mafuta ya petroli pia imepaa hadi kufikia sh 6,000 na 8,000 kwa lita moja.

Gharama nyingine ambazo hazikuwepo siku za nyuma pia zimepanda kutokana bei ya awali huku gharama ya kuchaji simu moja ni kati ya sh 1000 na 1500.

1 comment:

  1. JAMANI SERIKALI ILITAZAME KWA UPEO WA PEKEE HILI JAMBO LA SAMUNGE PENGINE BABU APEWE WASAIDIZI ZAIDI KUWASAIDIA WATU WANAOENDA HUKO. HII INADHIHIRISHA KUWA WATANZANIA WENGI NI WAGONJWA HASA MAGONJA HAYA YA KIZAZI KIPYA KAMA KISUKARI NA UKIMWI.SERIKALI IZIDI KUIMARISHA MAWASILIANO IKIWEZEKANA NCHI NZIMA WATU WAPATE TAARIFA YA KINACHOENDELEA SAMUNGE KWA BABU YETU. KULIKO HIZI ADHA ZINAZOJITOKEZA. WATU WATAZIDI KUUGUA ZAIDI ZAIDI NA PENGINE KUPOTEZA MAISHA KWANI WENGINE WANAACHA TIBA HOSPITALINI NA KUKIMBILIA SAMUNGE NA KUKUTA HALI WASIOITARAJIA HUKO.

    ReplyDelete